Bunge la Marekani lampinga Obama kuhusu kushtakiwa kwa Saudi Arabia

People hold up photos of victims during a memorial service at the 9/11 memorial on in New York. Haki miliki ya picha Getty Images

Rais wa Marekani Barack Obama amesema hatua ya bunge la nchi hiyo kupinga turufu yake dhidi ya mswada unaotoa fursa ya Saudi Arabia kushtakiwa kuhusiana na mashambulio ya 9/11 ni umeweka "mfano hatari".

Ameambia shirika la habari la CNN kwamba wabunge wamefanya "kosa".

Bunge la Congress lilipinga turufu ya Obama dhidi ya msawada huo ambao utatoa fursa kwa jamaa za waathiriwa wa shambulio la 9/11 kuwashtaki maafisa wa Saudi Arabia, hii ikiwa na maana kwamba sasa mswada huo utakuwa sheria.

Bunge la Seneti lilipiga kura 97-1 na Bunge la Wawakilishi 348-77.

Bw Obama amesema mswada huo utaweka kampuni za Marekani, wanajeshi na maafisa wa serikali katika hatari ya kushtakiwa nje ya nchi.

Mkurugenzi wa CIA John Brennan amesema kura hiyo ya wabunge ina "madhara makubwa" kwa usalama wa taifa.

Bunge la Congress limepitisha mswada huo unaofahamika kama Haki Dhidi ya Wafadhili wa Ugaidi (JASTA) mwaka huu licha ya Obama kuupinga.

Mswada huo, iwapo utakuwa sheria, basi utafanyia marekebisho sheria ya mwaka 1976 ambayo hukinga nchi nyingine dhidi ya kushtakiwa Marekani.

Hilo sasa litawapa nafasi jamaa za waathiriwa wa mashambulio hayo ya kigaidi ya mwaka 2001 yaliyosababisha vifo vya karibu watu 3000 kushtaki maafisa wa Saudi Arabia ambao wanashukiwa kuhusika.

Bw Obama, alipokuwa akikataa mswada huo, alisema hatua hiyo itaathiri uhusiano wa Marekani na Saudia na kuonya kwamba mataifa mengine yanaweza kujibu kwa kuwafungulia mashtaka maafisa wa Marekani wanaoshiriki vita Afghanistan na Iraq.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Bw Obama alisema: "Huu ni mfano hatari"

Bw Obama aliambia CNN Jumatano: "Huu unatoa mfano hatari na ni mfano bora wa ni kwa nini wakati mwingine inakubidi kufanya jambo lililo ngumu.

"Na kusema kweli, natumai Bunge la Congress lingechukua uamuzi ulio mgumu.

"Iwapo unafikiriwa ni kama unapiga kura dhidi ya jamaa za waathiriwa wa 9/11 muda mfupi kabla ya uchaguzi, si jambo la kushangaza, hilo ni jambo ngumu sana kwa watu kukubali.

"Lakini huo ungekuwa uamuzi mwafaka zaidi wa kuchukua."

Msemaji wa White House Josh Earnest ameambia wanahabari kwamba hilo ndilo "jambo la aibu zaidi ambalo Bunge la Seneti la Marekani" limefanya katika miongo mingi.

Lakini waliounga mkono sheria hiyo wanasema inaangazia vitendo vya kigaidi vilivyotekelezwa katika ardhi ya Marekani pekee.

"Ikulu ya White House na maafisa wa serikali kuu wanaangazia zaidi mambo ya kidiplomasia," amesema Seneta wa New York wa chama cha Democratic Chuck Schumer.

"Lakini sisi tunaangazia zaidi jamaa na haki."


Kura za turufu

  • George W Bush alitumia turufu kupinga miswada sawa na ya Bw Obama, 12, lakini turufu zake nne zilibatilishwa.
  • Bill Clinton alitumia turufu mara 37 na akashindwa mara mbili
  • Gerald Ford alipingwa mara 12
  • Rais wa karibuni zaidi wa Marekani ambaye hakuwahi kupingwa baada ya kutumia turufu ni Lyndon B Johnson
  • Anayeshikilia rekodi ni Andrew Johnson, ambaye kura zake za turufu zilipingwa mara 15 na Bunge la Congress alipokuwa rais miaka ya 1860.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii