Bei ya mafuta duniani yaanza kupanda baada ya maafikiano Opec

Oil pump Haki miliki ya picha AP

Bei ya mafuta duniani imeanza kupanda baada ya muungano wa mataifa yanayozalisha mafuta kwa wingi, Opec, kukubaliana kupunguza uzalishaji wa mafuta kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka minane.

Habari za kufikiwa kwa makubaliano hayo zimesababisha kupanda kwa bei ya mafuta ghafi kwa karibu asilimia 6.

Wanachama wa Opec wamekuwa wakilaumiana kusababisha mdororo wa bei ya mafuta kutoka nana wao kushindwa kuchukua msimamo mmoja wa kudhibiti bei.

Wanachama wa Opec wamekuwa wakikutana Algeria.

"Opec imechukua uamuzi wa kipekee leo," waziri wa mafuta wa Iran Bijan Zanganeh amesema.

Mafuta ghafi ya Brent, yanayotumiwa kama kigezo cha amfuta kimataifa, yalipanda bei na kufikia karibu asilimia 6 hadi $49 kila pipa baada ya tangazo hilo kutolewa.

Mawaziri wa mafuta wa nchi wanachama wamesema maelezo ya kina kuhusu mwafaka wa sasa yatajadiliwa kwenye mkutano mwingine Novemba.

Uzalishaji wa mafuta utapunguzwa hadi mapipa 700,000 kwa siku, ingawa upunguzaji wa uzalishaji hautakuwa sawa miongoni mwa wanachama.

Iran itaruhusiwa kuongeza uzalishaji wake.

Kulikuwa na suitafahamu awali baina ya Iran na mpinzani wake Mashariki ya Kati Saudi Arabia, jambo ambalo lilikuwa limezuia kupatikana kwa mwafaka.

Haki miliki ya picha Reuters

Wazalishaji wadogo wa mafuta walipigania kupunguzwa kwa uzalishaji baada ya mafuta kushuka bei kutoka $110 miaka miwili iliyopita.

Waziri wa mafuta wa Nigeria Ibe Kachikwu, taifa lililoathirika sana, alisema huo ni "mkataba mzuri sana".

Waziri wa kawi wa Algeria Algerian Noureddine Bouarfaa amesema uamuzi huo huo ulifikiwa kwa kauli moja.

Waziri wa kawi wa Qatar Mohammed Bin Saleh Al-Sada ambaye ndiye rais wa sasa wa Opec amesema uzalishaji sasa utakuwa kati ya mapipa 33.2 milioni na 33 milioni kwa siku.

Uzalishaji wa sasa unakadiriwa kuwa mapipa 33.3 milioni kwa siku.