Kenya inajenga reli nyingine ya 'wenye kichaa'?

Simba kwenye reli Haki miliki ya picha Nairobi Railway Museum

Maelfu ya watu waliokuwa wakitumiwa kujenga reli Kenya zaidi ya miaka 100 iliyopita walifariki wakijenga reli hiyo iliyobandikwa jina 'reli ya wenye kichaa'. Baadhi waliliwa na simba maeneo ya Tsavo.

Je, inawezekana kwamba Kenya inajenga reli nyingine ya 'wenye kichaa' isiyoelekea popote? Mwandishi wa BBC Alastair Leithhead anadadisi.

Kwenye Makumbusho ya Reli Nairobi, kuna kabati lenye kucha tatu za simba wawili ambao walihangaisha wajenzi.

"Waliua watu 100, lakini jumla ya waliofariki kutokana na maradhi na sababu nyingine ni 4,000. Hii ina maana kwamba kwa kila maili, watu wanne walifariki," anasema mhudumu katika makumbusho hayo, Elias Randiga.

Image caption Kucha za simba walioshambulia wajenzi wa reli miaka 100 iliyopita

Reli hiyo ya kwanza Kenya iliitwa "reli ya kichaa", na si kwa sababu tu kwamba watu waliliwa na simba, wakauawa na malaria na kushambuliwa na wenyeji ambao hawakutaka reli ipitie maeneo yao.

Sababu kuu ni kwamba ulikuwa mradi ghali sana kifedha na bunge la Uingereza lilisema ni "watu wenye kichaa pekee" wangetumia pesa nyingi hivyo kujenga reli isiyoenda popote pa maana.

Ujenzi ulianza 1896, na kuchangia kuchipuka kwa jiji la Nairobi.

'Mradi usio na manufaa'

Siku hizi, kujenga reli ni rahisi na hufanywa kwa kasi sana kwa kutumia teknolojia ya Wachina, lakini bado ni ghali mno.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Mbuga ya Taifa ya Nairobi ndiyo mbuga inayokaribia sana jiji duniani

Kenya imekopa mabilioni ya pesa na wakosoaji wa mradi huo wanauliza maswali yale yale yaliyoulizwa na wabunge wa Uingereza miaka ya 1800. Mbona inagharimu pesa nyingi hivi?

"Ni mradi usio na manufaa - hatuihitaji," anasema mchumi kutoka Kenya David Ndii.

"Haifai, gharama yake imeongezwa chumvi. Ndio mradi ghali zaidi ambao tumewahi kutekeleza na hauna maana kiuchumi sasa na hata siku zijazo."

Anaamini Kenya inajilimbikizia madeni sana, ikitekeleza miradi mikubwa ya miundo mbinu na ustawi, na pesa hizo hazitumiwi kwa uwazi.

Image caption Reli ya kisasa ya Kenya ikijengwa

Awamu ya kwanza kutoka Mombasa hadi Nairobi inakaribia kukamilishwa.

Lengo kuu ni kupunguza foleni au msongamano wa magari kwa kusafirisha mizigo mingi kwa kutumia reli na pia kusisimua ukuaji wa kiuchumi kwa kupunguza gharama ya kusafirisha mizigo.

Lakini wanaoupinga mradi huo wanaongezeka, hasa reli hiyo inapofikia awamu ambapo imepangiwa kupitia Mbuga ya Taifa ya Nairobi.

Wanaopinga ni pamoja na watetezi wa uhifadhi wa wanyama pori na mazingira, watu wa jamii ya Wamaasai pamoja na wale wanaoamini kwamba huu utakuwa mwisho wa mbuga pekee ya taifa ambayo inapatikana katika jiji duniani.

Kujenga madaraja

"Itabadilisha mbuga hii kabisa, haitakuwa pori tena," anasema Anthony Childs, aliye na hoteli ya kitalii inayopakana na Mbuga ya Taifa ya Nairobi.

Alituonyesha eneo ambalo awamu ya kwanza ya ujenzi tayari iliingia eneo la mbuga.

Msururu mrefu wa nguzo za saruji unaonekana ukisubiri kuwekewa reli juu yake. Na mitambo mizito inaendelea na kazi.

Image caption Ujenzi wa daraja la kupitishia reli hiyo Mbuga ya Taifa ya Nairobi umeanza

"Kwa hili, hawakushauriana nasi hata kidogo - walifanya hilo bila kutufahamisha," anasema.

"Mbuga hii ilikuwa maridadi mbeleni na haikuwa imeharibiwa," anasema Bw Childs.

"Mwanzo, walileta bomba la mafuta likapitia mbugani, kisha wakaleta boriti na kupitisha umeme, na sasa kuna reli. Hili litakoma lini?"

Kitili Mbathi, mkurugenzi mkuu wa Shirika la Huduma kwa Wanyamapori Kenya (KWS) majuzi alijaribu kuwatuliza waandamanaji waliokuwa wanapinga ujenzi wa reli hiyo, ambayo itajengwa kama daraja la umbali wa 6km (maili 3.7) kupitia mbuga hiyo.

"Tutashirikiana na mwanakandarasi kuhakikisha ujenzi haudhuru mazingira kadiri iwezekanavyo."

"Tumejipata kizungumkuti, tutoe hekari 50 za ujenzi wa reli na kuongeza gharama kwa asilimia 50, au kufuata njia hii isiyovuruga mambo sana ya kujenga daraja la kupitia mbugani," anasema Bw Mbathi.

KWS, pamoja na mtetezi wa uhifadhi wa mazingira na wanyamapori wa muda mrefu Richard Leakey, ambaye ndiye mwenyekiti, iliamua kusisitiza kujengwe daraja ndipo wanyama waweze kupita bila kutatizwa baada ya ujenzi kukamilika.

Ingawa ardhi ya mbuga hiyo si ya Wamaasai tena, wazee wa jamii hiyo wanasema ardhi hiyo ilikabidhiwa serikali ya wakoloni itumiwe kwa uhifadhi wa wanyama, na kwamba kujenga daraja ndani ni kuvunja mkataba huo.

Maandamano yameendelea, na rais alipokuwa anajiandaa kuzindua ujenzi wa awamu ya pili, mahakama ilisitisha ujenzi kwa muda kusubiri kusikizwa kwa ombi linalotaka madhara ya mradi huo kimazingira yatathminiwe kwa kina.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Wanaopinga ujenzi wa reli hiyo mbugani waliandamana jijini Nairobi

Pupa ya kukopa

Mchumi, Bw Ndii, anasema ana wasiwasi zaidi kutokana na pupa ya serkali kukopa pesa.

"Tayari tumeanza kuona athari za kukopa huku. Kulipa madeni kutakuwa kukichukua karibu nusu ya mapato ya serikali na miradi hii haileti mapato yoyote. Tunajiingiza katika mzozo wa kifedha utakaotuathiri miaka michache ijayo."

Reli hiyo ilipangwa iwe ya kuunganisha kanda, lakini nchi jirani sasa zinapanga miradi mingine ya reli ya bei nafuu.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Simba akipita karibu na magari Mbuga ya Taifa ya Nairobi 14 Julai, 2013.

Suala la iwapo ni "mradi wa kichaa" au "mradi wa busara" litategemea kiwango cha mizigo ambayo itapitishwa kwenye reli hii na kuhusu iwapo itakuwa heri kulipa deni la ujenzi miaka mingi ijayo.