Marekani kujenga kambi mpya ya kijeshi Niger

Marekani imeimarisha matumizi ya ndege zisizo na rubani chini ya utawala wa Rais Barack Obama Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Marekani imeimarisha matumizi ya ndege zisizo na rubani chini ya utawala wa Rais Barack Obama

Wizara ya Ulinzi ya Marekani imethibitisha kuwa, Marekani inajenga kambi kubwa ya jeshi la wanahewa nchini Niger, yenye uwezo wa kutumia ndege zisizo na rubani.

Kambi hiyo itagharimu takriban $100m.

Tayari uwepo wa Marekani katika mji mkuu wa nchi hiyo Niamey, umekuwepo kwa muda sasa, ambapo imekuwa ikitumia uwanja wa jeshi la angani, kwa pamoja na Ufaransa. Lakini kituo hicho kipya katika mji wa Agadez ulioko katikati mwa Niger, kitaipa Washington uwezo mkubwa wa kutumia ndege hizo, zisizo na rubani, ili kukabiliana na wapiganaji wenye itikadi kali kama vile Islamic State, katika mataifa jirani ya Libya, Mali na Nigeria.

Wachanganuzi wanasema kuwa, hatua hiyo ni njia mojawepo ya kupanua nguvu za kijeshi ya kukabiliana na operesheni ya kigaidi katika eneo hilo.