Somalia yailalamikia Marekani kuhusu mashambulio

Ndege
Maelezo ya picha,

Marekani imekuwa ikitumia ndege zisizo na rubani kushambulia al-Shabaab nchini Somalia

Serikali ya Somalia imeitaka Marekani kutoa ufafanuzi kuhusu shambulio ambalo lilitekelezwa na ndege za Marekani ambalo linadaiwa kusababisha vifo vya wanajeshi 22 pamoja na raia.

Marekani ilisema shambulio hilo, lililotekelezwa kwa kutumia ndege zisizokuwa na rubani katika jimbo la Galmudug, katikati mwa Somalia, liliua wapiganaji tisa wa kundi la Kiislamu la al-Shabab.

Maafisa wa serikali jimbo la Galmudug wamewatuhumu viongozi wa jimbo la Puntland, kwa kuwahadaa Wamarekani kwamba waliolengwa kwenye shambulio hilo walikuwa wanamgambo wa al-Shabab.

Kundi la Al-Shabab limesema hakuna mwanachama yeyote wa kundi hilo aliyeuawa.

Maelezo ya picha,

Kundi la al-Shabaab limesema hakuna wapiganaji wake waliouawa

Jeshi la Somalia limesema waliouawa walikuwa wanajeshi wa jeshi la jimbo la Galmudug.

Waandamanaji waliteketeza bendera ya Marekani huku mashambulio ya Marekani yakiendelea kwa siku ya pili Alhamisi mjini Galkayo.