Mwanajeshi wa India azuiliwa mateka Pakistan

Waziri Mkuu wa India Narendra Modi Haki miliki ya picha AFP/GETTY IMAGES
Image caption Waziri Mkuu wa India Narendra Modi amekabiliwa na shinikizo za kumtaka atume ujumbe mkali kwa Pakistan

India imesema mmoja wa wanajeshi wake anashikiliwa mateka na jeshi la Pakistan katika eneo la Kashmir linalodhibitiwa na Pakistan.

Hilo limejiri siku moja baada ya jeshi la India kusema lilikuwa limetekeleza mashambulio ya dhidi ya wanamgambo walio maeneo yanayodhibitiwa na Pakistan.

Habari ambazo hazijathibitishwa zinasema wanajeshi wa ardhini walihusika kwenye mashambulio hayo.

India imesema mwanajeshi anayezuiliwa mateka hakushiriki kwenye operesheni hilo bali aliingia kimakosa hadi maeneo yanayodhibitiwa na Pakistan.

Pakistan haijathibitisha kwamba inamzuilia mwanajeshi huyo, jambo ambalo wachanganuzi wanasema linaibua uwezekano kwamba huenda akarejeshwa kwa India kimyakimya.

Wasiwasi umekuwa ukiongezeka Kashmir siku za karibuni tangu wanamgambo waliposhambulia na kuua wanajeshi 18 wa India tarehe 18 Septemba.

India iliilaumu Pakistan lakini Pakistan ilikana kuhusika.

Mwandishi wa BBC aliyeko Delhi anasema pande zote mbili zinaonekana kuwa tayari kutozidisha uhasama kuhusu mwanajeshi huyo.

India na Pakistan zimekuwa zikidai umiliki wa eneo la Kashmir kwa miaka mingi lakini kwa sasa kila taifa humiliki sehemu ya eneo hilo lenye Waislamu wengi.

Nchi hizo mbili, ambazo zina silaha za nyuklia, zimepigana vita mara mbili kutokana na mzozo kuhusu Kashmir.