Mshukiwa wa ugaidi ahukumiwa miaka 80 jela nchini Kenya

Haki miliki ya picha AP
Image caption Abdi Rizzack Muktar Edow alihukumiwa kifungo cha miaka 20 jela alipopatikana na hatia ya kufadhili na kufanikisha ugaidi nchini Kenya

Mahakama moja nchini Kenya imemhukumu mshukiwa wa ugaidi kifungo cha miaka 80 jela.

Abdi Rizzack muktar Edow kwanza alihukumiwa kifungo cha miaka 20 jela alipopatikana na hatia ya kufadhili na kufanikisha ugaidi nchini Kenya.

Mfanyibiashara huyo mwenye umri wa miaka 24 alihukumiwa kifungo kingine cha miaka 10 kwa kila kosa, kwa makosa mengine sita ikiwemo kuwashawishi na kuwasajili vijana kujiunga na kundi hilo la kigaidi la nchini Somalia.

Hakimu mkuu bi Joyce Gandani alisema ni dhahiri kuwa Muktar Edow alikuwa na nia ya kuvuruga amani nchini Kenya kwa hivyo mbinu zote sharti zitumike kulinda maisha ya wakenya na maafisa wa usalama kutoka kwa watu wenye nia kama yake.

Image caption Pia alihukumiwa kifungo kingine cha miaka 10 kwa kila kosa, kwa makosa mengine sita ikiwemo kuwashawishi na kuwasajili vijana kujiunga na al shabab

Edow alikamatwa katika mbuga ya wanyama pori ya Maasai Mara Juni mwaka 2014 siku moja baada ya gari lake kunaswa na maafisa wa usalama likiwa limewabeba wapiganaji wa kundi la Al shabab walipoendesha uvamizi katika mji ulioko Kaskazini mwa Kenya Mandera.

Edow anaendesha biashara yakukodisha magari.

Mahakama iliambiwa kuwa Edow aliandaa kongamano la vijana katika msikiti uliogonga vichwa vya habari wa Musa ulioko Mombasa na kugawa video za kuwahamasisha vijana kujiunga na kundi hilo la kiislamu.

Kundi la wanamgambo wa kiislamu kutoka Somalia la al Shabab limekuwa likitekeleza mashambulizi nchini Kenya kwa lengo lakuishinikiza nchi hiyo kuondoa majeshi yake nchini Somalia baada ya kwenda kuisaidia serikali hafifu ya Mogadishu kujilinda dhidi ya makundi ya wanamgambo.