Teknolojia ya 3D kutumiwa kuunda nywele za binadamu

Mwanamke akishikilia nywele

Chanzo cha picha, Thinkstock

Maelezo ya picha,

Mabilioni ya pesa hutumiwa na watu wanaopoteza nywele

Kampuni moja nchini Ufaransa imesema kwamba teknolojia sawa na ile inayotumiwa kupiga chapa vitu vya uhalisia, 3D, huenda ikatumiwa kuunda nywele za binadamu na hivyo kufaa wenye upara.

Nywele hizo baadaye zitaweza kupandikizwa kwenye watu waliopoteza nywele.

Kampuni ya L'Oreal inashirikiana na kampuni ya kupiga chapa viumbe hai ya Poietis, ambayo imeunda teknolojia ya kupiga chapa kwa kutumia laser ambayo inaweza kuunda sehemu za seli za viumbe.

Vinyweleo vya nywele havijawahi kuundwa kwa njia hii awali lakini kampuni hizo mbili zinatarajia kwamba zitaweza kustawisha teknolojia na kuwezesha kuundwa kwa vinyweleo hivyo katika kipindi cha miaka mitatu ijayo.

Hata hivyo, shirika moja linaloangazia watu wanaopoteza nywele limesema bado ni mapema mno kwa watu kuanza kushangilia.

L'Oreal tayari hutumia ngozi iliyoundwa kwa teknolojia ya 3D kufanyia utafiti bidhaa za kutumiwa kwenye ngozi.

Chanzo cha picha, L'Oreal

Maelezo ya picha,

Mitambo inayotumiwa kuunda seli za viumbe