Ghasia zasababisha vifo vya watu 52 Ethiopia

Baadhi ya waliojeruhiwa Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Baadhi ya waliojeruhiwa

Waziri Mkuu wa Ethiopia Hailemariam Desalegn amewalaumu watu waliokuwa wakifanya fujo, kwa kusababisha mkanyagano katika jimbo la Oromiya, ambako amesema watu 52 wamefariki dunia.

Amekanusha ripoti kwamba, vikosi vya jeshi vimefyatua risasi katika tamasha la kidini lililokuwa likihudhuriwa na mamia kwa maelfu ya watu.

Mashuhuda wa tukio hilo wanasema ghasia zilianza wakati Waandamanaji walipo ingilia kati hotuba za maafisa katika tamasha hilo katika mji wa Bishoftu.

Upinzani nchini humo unasema takriban watu 100 wamekufa. Wengi ya watu hao, walikufa baada ya kuangukia kwenye korongo, wakati wakijaribu kukimbia.

Wakazi wa mkoa huo pamoja na jimbo la jirani la Amhara, kwa miezi kadhaa wameshuhudia ghasia zilizosababisha vifo wakati wenyeji wa maeneo hayo wakipambana na kile walichokiita kuongezeka kwa ukandamizaji unaofanywa na serikali kuu.