Kim Kardashian aporwa mali ya mamilioni ya euro Paris

Kim Kardashian na mumewe Kanye West Haki miliki ya picha Other
Image caption Kim Kardashian na mumewe Kanye West

Nyota wa televisheni nchini Marekani Kim Kardashian ameporwa vito vya mamilioni ya pesa na watu wenye silaha waliomvamia katika hoteli moja mjini Paris.

Polisi wanasema ameibiwa vito vya euro milioni kadha. Wizi huo ulitokea mwendo wa saa tisa usiku wa manane.

Msemaji wake Ina Treciokas anasema nyota huyo wa uigizaji wa vipindi vya maisha ya uhalisia alizuiliwa na watu wawili waliokuwa wamejifanya maafisa wa polisi na ambao walikuwa wamejifunika nyuso zao.

"Ameshtushwa sana na tukio hilo lakini hajaumizwa," msemaji wake amesema.

Haki miliki ya picha Getty Images

Mumewe Kanye West amekatisha ghafla tamasha ambayo amekuwa akishiriki mjini New York.

Kanye West alikuwa akitumbuiza katika tamasha ya Meadows Music and Arts Festival na amesitisha ghafla utumbuizaji na kuwaambia mashabiki kwamba alikuwa na "dharura ya kinyumbani".

"Nawaomba radhi, nina dharura ya kinyumbani na inanibidi kukomea hapa kwa sasa," West aliwaambia mashabiki.

Kardashian West, 35, alikuwa ameenda Paris, pamoja na mamake Kris Jenner na dadake Kendall Jenner, kuhudhuria maonyesho ya mitindo.

Alihudhuria maonyesho ya Givenchy Jumapili jioni.

Haki miliki ya picha Other
Image caption Vitalii Sediuk, ambaye amewahi kuwakabili Gigi Hadid na Leonardo DiCaprio alijaribu kubusu makalio ya Kardashian wiki iliyopita

Wiki iliyopita, alikabiliwa na Vitalii Sediuk, mtu mwenye mazoea ya kukabili watu mashuhuri alipokuwa akijaribu kuingia kwenye mgahawa.

Paris ni mji unaopendwa sana na Kardashian na mumewe.

Wawili hao walikaa mjini humo wikendi iliyotangulia kabla yao kufunga ndoa mjini Florence Mei 2014.

Haijabainika iwapo watoto wa wawili hao, North mwenye umri wa miaka 3 na Saint mwenye umri wa miezi 10, walikuwa kwenye hoteli hiyo na Kardashian.