Programu mpya ya Facebook kuzinduliwa Kenya

Watu bilioni moja duniani hutumia programu ya Messenger kila mwezi kwa mujibu wa Facebook Haki miliki ya picha FACEBOOK
Image caption Watu bilioni moja duniani hutumia programu ya Messenger kila mwezi kwa mujibu wa Facebook

Facebook imezindua aina mpya ya programu tumishi yake ya kutuma ujumbe ambayo inawalenga watu wa mataifa yanayoendelea.

Programu hiyo mpya ya Messenger, ambayo inaitwa Messenger Lite, itaanza kutumiwa nchini Kenya, Tunisia, Malaysia, Sri Lanka na Venezuela kwanza.

Itazinduliwa katika nchi nyingine baadaye.

Messenger Lite imeundwa kutotumia sana data, jambo ambalo huwa tatizo kubwa mataifa yanayoendelea kutokana na gharama pamoja na kasi ya mtandao.

Programu hiyo ya simu za Android pia inaweza kufanya kazi kwa urahisi maeneo ambayo huduma ya mtandao si ya kutegemewa.

"Messenger Lite ukubwa wake ni chini ya 10MB, hivyo ni rahisi sana kuiweka kwenye simu na kuifungulia," taarifa ya Facebook imesema.

"Inatumia nembo inayokaribiana na ya Messenger, lakini rangi zake ni kinyume."

Wanaotumia programu hiyo ya Messenger Lite kwenye simu zao bado wataweza kutumia huduma muhimu zikiwemo uwezo wa kutuma ujumbe, picha na vihusishi vya kurasa za mtandao.

Hata hivyo, hawataweza kupiga simu za kawaida au za video kwa kutumia programu hiyo kama ilivyo kwa programu za kawaida za Messenger.

Facebook pia huwa na aina 'nyepesi' ya programu tumishi ya Facebook ambayo huitwa Free Basics na ambayo hufaa sana watu wasio na huduma ya kutegemewa ya mtandao.

Programu hiyo hupatikana katika mataifa kadha.

Afisa mkuu mtendaji wa Facebook Mark Zuckerberg mara kwa mara amekuwa akisema lengo ya kampuni yake ni kuhakikisha kila mtu duniani anaweza kutumia huduma ya mtandao.

Inakadiriwa kwamba watu bilioni moja duniani hutumia programu ya Messenger kutuma au kupokea ujumbe kila mwezi.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii