Polisi wawakamata watu 40 wa jamii ya Oromo Kenya

Watu kadhaa nchini Ethiopia ambao walikuwa wakifanya maandamano ya kuipinga serikali walifariki katika makanyagano
Image caption Watu kadhaa nchini Ethiopia ambao walikuwa wakifanya maandamano ya kuipinga serikali walifariki katika makanyagano

Maafisa wa polisi nchini Kenya wamewakamata watu 40 wa jamii ya Oromo kwa kufanya maandamano kinyume na sheria katika mji mkuu wa Nairobi,kulingana na gazeti la Daily Nation.

Gazeti hilo limemnukuu afisia mkuu wa polisi wa eneo la Gigiri Vitalis Otieno akisema kuwa maafisa wa polisi waliitwa katika eneo hilo baada ya kundi hilo kuzua ghasia.

''Wengine wao wako nchini kinyume na sheria...tunawachunguza na kukagua nakala zao'',aliongezea.

Kiongozi wa kundi hilo hatahivyo amesema kuwa waliwaelezea maafisa wa kaunti kuhusu mkutano huo mnamo tarehe 29 mwezi Septemba ,2016 na kulipa fedha zinazohitaji za shilingi 3000 kwa mujibu wa ripoti hiyo.

Mkutano huo unafuatia ripoti za watu kutoka kwa jamii ya Oromo ambao inadaiwa kuwa waliuawa katika mkanyagano wakati wa maandamano siku ya Jumapili nchini Ethiopia.