Wapinga dhamana ya kuachiliwa kwa Waoromo Kenya

Raia wa Oromo waliokamatwa wakisherehekea siku ya Irecha Kenya
Image caption Raia wa Oromo waliokamatwa wakisherehekea siku ya Irecha Kenya

Viongozi kutoka kwa jamii ya Oromo nchini Kenya wamepinga kuhusu dhamana ya juu ya dola 500 ya kuachiliwa kwa kila mmoja wa raia wa jamii hiyo ambaye alishtakiwa kwa kufanya mkutano kinyume cha sheria mjini Nairobi.

Walikongamana katika bustani ya Uhuru Park kusherehekea utamaduni wa jamii hiyo kwa jina Irecha na walikamatwa siku ya Jumapili kwa kufanya mkutano usio halali.

Wakili wao Stanley King'ahi alikana mashtaka dhidi yao na kutoa risiti zilizoonyesha kwamba wateja wake walilipa serikali ya kaunti ili kuutumia uwanja huo.

Kukamatwa kwao kunajiri siku ambayo raia 52 wa Oromo waliuawa nchini Ethiopia wakati wa maandamano ya sherehe za Irecha.