Duterte asema Obama anaweza 'kwenda jehanamu'

John Jansen, Andre Costales na Maximo Ballesteros Manila Oktoba 4, 2016. Haki miliki ya picha AFP/Getty Images
Image caption Mazoezi ya sasa ya kijeshi yanatarajiwa kuimarisha uwezo wa majeshi hayo kushughulikia dharura na pia kuimarisha uhusiano

Rais wa Ufilipino Rodrigo Duterte amerejelea tena shutuma zake dhidi ya Rais Obama na viongozi wengine wa nchi za Magharibi wanaopinga mpango wake wa kupambana na walanguzi wa dawa za kulevya.

Kiongozi huyo amesema Bw Obama anaweza "kwenda jehanamu".

Umoja wa Ulaya, ambao pia umemkosoa Bw Duterte, unaweza "kuchagua kwenda eneo la kutakasia dhambi ndogo, kwa sababu jehanamu kumejaa", amesema.

Watu karibu 3,000 wameuawa tangu kiongozi huyo alipoingia madarakani mwezi Juni.

Watu wanaoshukiwa kulangua mihadarati au kuwa waraibu wa dawa hizo wamekuwa wakiuawa na maafisa wa polisi na magenge yanayoungwa mkono na serikali.

Bw Duterte amesema Urusi na China wako tayari kuwa washirika wake.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Bw Duterte

Wanajeshi wa Ufilipino na Marekani kwa sasa wanafanya mazoezi ya pamoja ya kijeshi lakini Bw Duterte amesema mazoezi hayo hayana manufaa kwa raia wa Ufilipino.

Msemaji wa ikulu ya White House Josh Earnest amesema Washington kufikia sasa haijapokea ombi lolote rasmi kutoka kwa Ufilipino kufanyia marekebisho mikataba ya ushirikiano baina ya nchi hizo mbili.

Akiwahutubia maafisa wa serikali na wafanyabiashara, Bw Duterte amesema amesikitishwa sana na Marekani kwa kukosoa mbinu za Ufilipino za kukabiliana na mihadarati.

Ameeleza Marekani kama mshirika asiye wa kutegemewa.

"Badala ya kutusaidia, wizara ya mambo ya nje (ya Marekani) ndio wa kwanza kutukosoa, kwa hivyo wanaweza kwenda jehanamu, Bw Obama, unaweza kwenda jehanamu."

Baadaye Jumanne, alitahadharisha kwamba: "Mwishowe huenda, nikiwa bado uongozini, nikajitenga na Marekani. Heri kwenda kwa Urusi au Uchina."

Aidha, Bw Duterte amefichua kwamba Marekani imekataa kiuzia silaha serikali yake lakini akaongeza kwamba watazinunua kwingine.

"Iwapo hamtaki kuuza silaha, nitaenda Urusi. Niliwatuma majenerali Urusi na Urusi walisema, 'Msiwe na wasiwasi, tuna kila kitu mnachohitaji, tutawapa'.

"Kuhusu China, walisema, 'Njooni na mtie saini na kila kitu kitafikishwa kwenu'," Rais Duterte amesema.

Ufilipino ilikuwa koloni ya Marekani na imekuwa mshirika mkuu Asia mashariki.

Haki miliki ya picha Associated Press
Image caption Wanaharakati waliandamana nje ya ubalozi wa Markani, Manila adhidi ya ushirikiano wa kijeshi kati ya Ufilipino na Marekani
Haki miliki ya picha AFP/Getty Images
Image caption Zaidi ya wanajeshi 1,100 wa Marekani wanashiriki mazoezi ya pamoja na wanajeshi wa Ufilipino. Huyu hapa ni kamanda mkuu wa jeshi la wanamaji la Ufilipino Meja Jenerali Andre Costales akitoa hotuba wakati wa uzinduzi wa mazoezi ya sasa Manila

Wanajeshi 1,100 wa Marekani na 400 wa Ufilipino wanashriiki mazoezi hayo ya pamoja ya kijeshi ambayo yataendelea kwa siku nane.

Uhusiano baina ya Marekani na Ufilipino ulidorora mwezi uliopita baada ya Rais Duterte kuonekana kumtusi Rais Obama.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii