Afungiwa nyumbani kwa miaka 30

Wazazi wa mwanamme wa miaka 43 wanachunguzwa na polisi huko Bavaria, Ujerumani Haki miliki ya picha AP
Image caption Mwanamme wa miaka 43 hawajahi kuonekana hadharani kwa miaka30

Polisi nchini Ujerumani wanawachunguza mume na mke ambao wanadaiwa kumfungia mwanao wa kiume ndani ya nyumba kwa miaka 30, katika jimbo la Bavaria

Mwanamme huyo wa miaka 43 hajawahi kuonekana hadharani tangu kuacha shule akiwa na miaka 13. Polisi wamesema japo mwanamme huyo yuko shwari kiafya, hata hivyo ameonekana kuwa na mfadhaiko.

Hata hivyo wamesema hawatawasilisha mashtaka yeyote. Polisi walijulishwa kuhusu tukio hilo na jirani ya mtu huyo ambapo walimchukua kutoka nyumba alikoishi na kumpeleka hospitalini.

Hata hivyo walikabiliwa na wakati mgumu kumshawishi bwana yule kupelekwa hospitailini. Mamake amesema mwanawe huyo hakufungiwa na kwamba ni yeye binafsi aliyekataa kwenda shule na kuamua kusalia ndani ya nyumba kwa miaka 30.

Image caption Kisa hicho kilitokea kijiji cha Bayreuth, jimbo la Bavaria

Maafisa wa hospitali alikolazwa wanajaribu kumfanyia uchunguzi wa kiakili. Wengi wanahoji kuhusu jinsi mtu huyo aliepuka ushawishi wa mitandao, ujana, huduma za kijamii na zile za kiafya bila kujulikana.