Mambo 10 muhimu kuhusu reli mpya Ethiopia

Reli ya umeme
Image caption Reli hiyo inaunganisha Addis Ababa na mji wa Djibouti

Reli mpya ya aina yake inayounganisha mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa na mji mkuu wa Djibouti imezinduliwa.

Naibu waziri mkuu wa China Wang Yang miaka mitatu iliyopita alisema mradi huo wa reli ni kama "Tazara ya enzi mpya," kwa mujibu wa shirika la habari la serikali ya China la Xinhua.

Haya hapa ni mambo kumi muhimu kuhusu reli hiyo:

1. Reli hiyo mpya ina urefu wa kilomita 752 na inatoka Addis Ababa hadi bandari ya Doraleh katika mji wa Djibouti, kwenye ghuba ya Aden. Itasafirisha abiria na mizigo. Sehemu kubwa ya reli hiyo imo Ethiopia, Kilomita 652 kutoka Addis Ababa hadi Dewale mpakani, na sehemu iliyosalia Djibouti.

Image caption Uzinduzi wa reli hiyo umefanyika leo mjini Addis Ababa

2. Reli hiyo inatoka eneo lililo mita 2,400 juu ya usawa wa bahari hadi baharini. Hilo lilikuwa changamoto kiteknolojia wakati wa ujenzi.

3. Ndiyo reli ya kwanza kabisa Afrika kusini mwa jangwa la Sahara - ukiondoa Afrika Kusini - ambayo inatumia kikamilifu nguvu za umeme. Umeme utatoka kwa nyaya zinazopitia juu.

4. Reli hiyo imejengwa kuwezesha treni kwenda kwa kasi ya kilomita 120 kwa saa. Imejengwa kwa kufuata karibu njia sawa na iliyofuatwa na reli iliyojengwa na Wazungu zaidi ya miaka 100 iliyopita.

5. Reli hiyo inatarajiwa kupunguza muda wa kusafirisha mizigo kutoka zaidi ya siku mbili hadi takriban saa nane.

6. Gharama ya ujenzi wa reli hiyo ni dola 4 bilioni za Marekani. Ufadhili umetoka kwa benki ya serikali ya China ya Exim & Import (70%) na sehemu iliyosalia kutoka kwa serikali ya Ethiopia. Ujenzi umefanywa na kampuni mbili zinazomilikiwa na serikali ya China, China Railway Group na China Civil Engineering Construction Corporation.

Image caption Treni zitakazotumia reli hiyo zitasafirisha mizigo na abiria

7. Reli hiyo ndio mradi wa pili mkubwa wa reli inayounganisha mataifa zaidi ya mawili ambayo imejengwa na kampuni za Kichina barani Afrika. Mradi huo mwingine ni reli ya Tazara inayounganisha jiji la Dar es Salaam, Tanzania na mji wa Kapiri Mposhi nchini Zambia.

Wakati wa ziara yake Ethiopia Mei 2013, naibu waziri mkuu wa China Wang Yang alisema mradi huo wa reli wa Ethiopia-Djibouti ni "Tazara ya enzi mpya," kwa mujibu wa shirika la habari la serikali la Xinhua.

Kinyume na mradi wa Tazara, ambao ulijengwa miaka ya 1970 kama mradi wa msaada wa kimataifa kutoka kwa serikali ya Uchina, reli hiyo ya Ethiopia-Djibouti ni mradi wa kibiashara kati ya kampuni za Kichina na serikali za mataifa hayo mawili ya Afrika.

Image caption Ethiopia imepanga kujenga reli za kisasa za jumla ya umbali wa kilomita 5,000

8. Ujenzi wa reli hiyo umechukua miaka sita.

9. Katika baadhi ya maeneo, kumejengwa madaraja ya kuwezesha wanyama kupitia chini.

10. Reli hiyo itasimamiwa na ubia wa kampuni za China kwa miaka sita hivi kutokana na kutokuwepo kwa watu wenye ujuzi wa kusimamia reli ya aina hiyo. Ubia wa kampuni hiyo utawapa mafunzo wenyeji katika kipindi hicho.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii