Rafia yainua kipato cha wanawake Tanzania

Wanawake wakiwa wanavuna Rafia
Maelezo ya picha,

Wanawake wakiwa wanavuna Rafia

Ukulima wa Rafia unazidi kushamiri maeneo yanayozunguka msitu wa Nou uliopo mkoa wa Manyara, kaskazini mwa Tanzania.

Kilimo hiki kinacholimwa kwenye vyanzo vya maji kinafahamika kwa jina la Rafia, ama "sawa" kwa lugha ya wenyeji wa hapo ambao ni wairaq.

Majani ya Rafia yamewawezesha wanawake wa hapo kuweza kujipatia kipato na kuacha kuharibu mazingira ya msitu wa Nou.

Maelezo ya picha,

Kikundi cha Tsawawi,Babati

Miaka ya nyuma akina mama wengi nchini Tanzania walijihusisha na shughuli za ususi, ufumaji na ushonaji kwa kutuma mikono lakini sasa hali ni tofauti, haswa maeneo ya mjini na hii ni kutokana na kukua kwa teknolojia ambayo imefanya shughuli hizi kupotea maeneo mengi.

Hali ambayo ni tofauti kabisa katika maeneo yanaouzunguka msitu wa Nou,Wanawake wa maeneo haya wanajivunia kupata kipato chao wenyewe kutokana na shuguli hii ya ususi wa vikapu, mikeka na mapambo mbali mbali.

Ubunifu wa wanawake hawa, ambao walipata mafunzo kutoka kwa shirika lisilo la kiserikali liitwalo Farm Afrika, umewakomboa kutoka kwa minyororo ya utegemezi na sasa wana kipato cha kujikidhi kimaisha na vile vile kuchangia kiuchumi nyumbani tofauti na miaka ya nyuma walipokua wakitegemea waume wao kwa kila kitu maishani mwao..