Kylie Minogue kusubiri ndoa za wapenzi wa jinsia moja Australia

Mwigizaji Mwingereza Joshua Sasse na mwanamuziki wa Australia Kylie Minogue Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Mwigizaji Mwingereza Joshua Sasse na mwanamuziki wa Australia Kylie Minogue

Mchumba wa mwanamuziki maarufu kutoka Australia Kylie Minogue amesema wameahirisha harusi yao hadi pale ndoa za jinsia moja zitakapohalalishwa nchini Australia.

Minogue, 48, na mwigizaji Mwingereza Joshua Sasse, 28, walitangaza uchumba wao mapema mwaka huu.

Wawili hao wamekuwa wakitetea haki sawa za kufunga ndoa nchini Australia.

Serikali nchini humo imependekeza kuandaliwa kwa kura ya maamuzi kuhusu kuhalalishwa kwa ndoa za wapenzi wa jinsia moja Februari 2017.

Haki miliki ya picha Kylie Minogue/Instagram
Image caption Kylie Minogue akiwa amevalia fulana yenye ujumbe "Say I Do Down Under" ya kuunga mkono haki za wapenzi wa jinsia moja kufunga ndoa

Bw Sasse amesema angependa wafunge ndoa mjini Melbourne lakini hawatafanya hivyo "hadi sheria hii ipitishwe nchini Australia".

Amesema alishangaa sana alipogundua kwamba ndoa za wapenzi wa jinsia moja hazikubaliwi kisheria nchini humo.

Kura hiyo ya maamuzi itagharimu jumla ya A$160m (£95m; $120m) ambazo zinajumuishwa pia pesa za kufadhili kampeni za wanaounga mkono na wanaopinga.