US 'yaishutumu' Israel kuhusu makaazi mapya

Eneo la West bank linalozozaniwa
Image caption Eneo la West bank linalozozaniwa

Serikali ya Marekani imeshutumu vikali hatua ya Israel ya kuidhinisha mipango mipya ya ujenzi wa nyumba katika eneo la West Bank.

Ikulu ya White House na wizara ya maswala ya kigeni imesema kuwa mipango ya kujenga nyumba mpya 300 pamoja na eneo la viwanda inaathiri shughuli za kuwepo kwa mataifa mawili yalio huru kufuatia migogoro kati ya Israel na Palestina.

Israel imesisitiza kuwa ni ujenzi wa chini ya nyumba 100 ulioidhinishwa.

Waziri wake wa maswala ya kigeni amesema kuwa nyumba mpya zitajengwa katikati ya maeneo ya makaazi yaliopo.

Takriban raia 570,000 wa Israel wanaishi katika zaidi ya nyumba 100 zilizojengwa tangu Israel ikalie maeneo hayo yaliopo katika eneo la West Bank na Mashariki mwa Jerusalem mwaka 1967.

Makaazi hayo yanatajwa kuwa haramu chini ya sheria ya kimataifa,ijapokuwa Israel inapinga hilo.

Mnamo mwezi Juali,mataifa yenye uwezo mkubwa duniani yalionya kuhusu mgogoro wa mara kwa mara kati ya Israel na Palestina kutokana na makaazi hayo.