Njiwa akamatwa na kuzuiliwa na polisi India

Njiwa Haki miliki ya picha AP

Polisi nchini India wanasema walimkamata na kumzuilia njiwa mmoja ambaye alipatikana akiwa amebeba ujumbe wa kumtishia waziri mkuu wa nchi hiyo.

Ndege huyo alipatikana karibu na mpaka wa nchi hiyo na Pakistan.

"BSF [Polisi Walinzi wa Mpakani] walimpaka akiwa na karatasi yenye ujumbe ulioandikwa kwa lugha ya Urdu ukisema: 'Modi, hatujakuwa watu sawa tangu 1971. Sasa, kila mtoto yuko tayari kupigana na India," mkuu wa polisi wa Pathankot, Bw Rakesh Kumar, aliambia AFP kwa simu.

Waziri mkuu Narendra Modi alichaguliwa 2014 na tangu wakati huo ameongeza matumizi ya kuimarisha jeshi la India.

Bado kuna mkataba wa kusitisha mapigano uliotiwa saini mwaka 2003 kati ya India na Pakistan, lakini mara kwa mara mataifa hayo hulaumiana kwa kuukiuka.

Maafisa wanasema ndege huyo alipatikana Pathankot katika jimbo la kaskazini la Punjab, ambapo wanamgambo wenye ngome yao Pakistan walitekeleza shambulio dhidi ya kambi ya jeshi la wanahewa la India mwezi Januari.

Haki miliki ya picha Reuters

Mara ya wisho nchi hizo mbili kupigana vita kamili ilikuwa mwaka 1971.

Mwaka uliopita, njia mwingine alikamatwa na polisi akishukiwa kuwa jasusi kutoka Pakistan.