Kimbunga Matthew chaua watu 300 Haiti

Majengo mengi pia yameporomoka Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Mamia ya watu wamekufa baada ya Kimbunga Mathew kupiga Haiti

Idadi ya vifo kufuatia kimbunga Matthew nchini Haiti inakaribia watu 300, kwa mujibu wa serikali.

Katika Mji wa Jeremie asilimia 80 ya majengo yameporomoka.

Hadhi ya Kimbunga Matthew kwa mara nyingine imepandishwa hadi ngazi ya nne, hatua ambayo ndiyo ya pili kwa ukubwa katika mgawanyo wa aina mbali mbali za Kimbunga, huku kikielekea katika jimbo la Florida nchini Marekani.

Maafisa wa serikali ya Haiti wametoa takwimu mpya kuhusiana na maafa yaliyosababisha na kimbunga hicho.

Siku ya alhamisi, serikali ya nchi hiyo ilisema watu mia moja tayari walikuwa wamepoteza maisha yao.

Haki miliki ya picha AFP/GETTY
Image caption Watu wengi wamepoteza makao nchini Haiti

Kimbunga Matthew ambacho ndicho kubwa zaidi katika visiwa vya Caribbean kwa zaidi ya muongo mmoja uliopita, kimepiga taifa la Bahamas baada ya kupitia Haiti na Cuba.

Wengi wa waliopoteza maisha nchini Haiti, walikuwa wakiishi mjini na vijiji vinavyojulikana kwa shughuli za uvuvi katika maeneo ya pwani ya kusini.

Wengi walifariki baada ya kuangukiwa na miti, taka zilizokuwa zikisombwa au hata kusombwa na maji, baada ya mito nyingi kuvunja kingo zao.

Kimbunga hicho kiliambatana na upepo uliokuwa ukivuma kwa kasi ya hadi kilomita 280 kwa saa.

Haki miliki ya picha Reutes
Image caption Marekani imeahidi kutuma helikopta tisa za kusaidia katika uokoaji

Usafiri kati ya maeneo ya kusini Magharibi na meneo mengine nchini Haiti ulisitishwa baada ya daraja moja muhimu inayounganisha maeneo hayo kusomba na maji.

Mashirika yasiyo ya kiserikali yamesema kwa sasa hakuna huduma za simu na umeme na kuwa watu wanapungukiwa na vyakula na maji safi ya kunywa.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Nyumba nyingi zimeharibiwa kabisa nchini Haiti

Mratibu wa umoja wa mataifa anayehusika na masuala ya misaada ya kibinadam amesema kuwa zaidi ya watu laki tatu na nusu wanahitaji misaada ya kibinadamu.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii