Mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel 2016 kutangazwa

Mshindi atatangazwa mwendo wa saa sita mchana saa za Afrika Mashariki Haki miliki ya picha AP
Image caption Mshindi atatangazwa mwendo wa saa sita mchana saa za Afrika Mashariki

Mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel wa mwaka 2016 anatarajiwa kutangazwa leo mjini Oslo, Norway.

Mshindi atatoka kwenye orodha ya watu na mashirika 376.

Miongoni mwa wanaoshindania tuzo hiyo, 228 ni watu binafsi na 148 ni mashirika.

Hata hivyo, mshindi huwekwa kuwa siri kubwa na mara nyingi chaguo limekuwa likishangaza watu.

Licha ya usiri mkuu, kuna wanaopigiwa upatu ambao ni pamoja watoaji huduma wa White Helmets nchini Syria na wakuu waliosaidia kupatikana kwa mkataba wa nyuklia kati ya nchi za Magharibi na Iran.

Kumekuwa pia na watu ambao wengi hawawatarajii washinde, lakini bado wanatajawa na baadhi, miongoni mwao akiwa Donald Trump kwa juhudi zake za "kutafuta amani kupitia nguvu za falsafa."

White Helmets ni wahudumu wa kujitolea Syria ambao husaidia kuwatoa waathiriwa kutoka kwa vifusi vya majumba yaliyoshambuliwa kwa mabomu.

Ombi la kuwatetea washinde tuzo hiyo limeungwa mkono na watu 304,000.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption White Helmets ni miongoni wa wanaopigiwa upatu kushinda

Tuzo ya mwaka jana iliwaendea watu wanne walioshiriki katika mazungumzo ya kitaifa Tunisia na kusaidia taifa hilo kuingia mfumo wa kidemokrasia.

Wengi walitarajia kansela wa Ujerumani Angela Merkel angeshinda kwa juhudi zake kusaidia wahamiaji wanaoingia Ulaya.