Miaka 115 ndio 'mwisho wa maisha' kwa binadamu

Kuzeeka Haki miliki ya picha iStock

Wanasayansi nchini Marekani wamesema baada ya kufanya utafiti wamegundua huenda umri mkubwa zaidi ambao binadamu anaweza kuishi duniani ni miaka 115.

Matokeo ya utafiti huo yamechapishwa katika jarida la Nature.

Wamefikia uamuzi huo baada ya kutathmini data zilizokusanywa kwa miaka mingi kuhusu maisha ya mwanadamu.

Wanasema kunao watu wanaoweza kubahatika waishi miaka kadha zaidi ya 115 lakini utakaa sana kabla ya kupata mtu hata mmoja aliyefikisha umri wa miaka 125.

Wanasema utahitaji "kutafuta katika sayari 10,000 za dunia" kupata angalau binadamu aliyeishi miaka 125.

Lakini baadhi ya wanasayansi wamekosoa utafiti huo, na baadhi hata wakautaja kama dhihaka.

Umri wa binadamu kuishi umekuwa ukiongezeka tangu kuanza kwa karne ya kumi na tisa kutokana na kugunduliwa kwa chanjo, wanawake kujifungua kwa njia salama zaidi na juhudi za kukabiliana na maradhi kama vile saratani na maradhi ya moyo.

Lakini umri unaweza kuendelea kuongezeka?

Kundi hilo la watafiti kutoka New York lilichunguza data kutoka kwa Hazina Data ya Vifo vya Binadamu na vifo vya watu waliozidi umri wa miaka 110 Japan, Ufaransa, Uingereza na Marekani.

Wanasema uchunguzi wao ulibaini ongezeko la umri wa kuishi miongoni mwa wale wazee kabisa ni kama umefikia upeo.

Prof Jan Vijg, mmoja wa watafiti anayetoka Chuo Kikuu cha Matibabu cha Albert Einstein, aliambia BBC News: "Miongoni mwa watu wa umri wa miaka 105 na zaidi, hakujakuwa na mabadiliko makubwa, na hili linakuonyesha kwamba tunafikia upeo wa maisha ya binadamu.

"Kwa mara ya kwanza katika historia, tumeweza kuona hili, upeo huu, ambao ni miaka 115."

Mtu aliyeishi miaka mingi zaidi

Haki miliki ya picha Alamy
Image caption Jeanne Calment

Jeanne Calment ndiye binadamu ambaye anatambuliwa kuwa aliyeishi miaka mingi duniani na ambaye kuna stakabadhi rasmi za kuthibitisha hilo.

Alikuwa na miaka 122 alipofariki 1997.

Tangu wakati huo, hakuna aliyekaribia umri huo.

Dhihaka?

Prof James Vaupel, mkurugenzi wa taasisi ya utafiti kuhusu watu ya Max Planck ni mmoja wa wanaopinga utafiti huo.

Anasema zamani, wanasayansi walikuwa wamedai umri wa juu zaidi anaoweza kuishi binadamu ni miaka 65, wakaenda kwa 85 na baadaye wakasema miaka 105 lakini historia ilidhihirisha baadaye kwamba walikuwa wamekosea.

"[Utafiti huu] hauongezi ujuzi wowote kuhusu tutaishi kwa muda gani."

Utafiti, ambao umeangazia wanyama, hata hivyo umedokeza huenda kukawa na upeo kwa maisha ya viumbe.

Prof Jay Olshansky, wa Chuo Kikuu cha Illinois, anasema panya huishi siku 1,000, na mbwa siku 5,000 hivi na "binadamu huenda wanakaribia upeo wa uwezo wao wa kuishi".

Kuzuia uzee?

Changamoto kuu ni kwamba binadamu hajaweza kupata mbinu ya kuendelea kuishi baada ya kuzeeka sana.

Hili sana huamuliwa na maelezo kwenye chembenasaba au DNA.

Kwa hivyo, juhudi zozote za kuongeza umri wa binadamu kuishi zitahitaji kufanya jambo la ziada na si tu kutibu magonjwa.

Juhudi hizo zitahitajika kupata njia ya kuzuia kuzeeka kwa kila seli ndani ya mwili.

Prof Jan Vijg ameongeza: "Ili kuwezesha watu kuishi miaka 120, 125 au 130 labda, tutahitaji kufanya ugunduzi mkubwa."

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii