Flamingo wapungua kwa kiwango cha kuogofya Kenya

Flamingo
Image caption Ndege aina ya Flamingo katika ziwa Nakuru

Ndege aina ya flamingo, ambao pia hujulikana kama korongo, wamepungua kwa zaidi ya asilimia 50 nchini Kenya, kutokana na mabadiliko ya hali ya anga ambayo yamewafanya ndege hao kuhama mbuga la ziwa Nakuru.

Ndege hao aina ya flamingo yenye rangi ya poda, kwa hivi sasa wako kama 2,000 na siyo kama ilivyokuwa hapo awali ambapo ilikadiriwa kwamba kulikuwa na hadi flamingo 1.5 milioni katika mbuga hiyo.

Image caption Msimamizi wa mbuga ya ziwa Nakuru Bw Dickson Ritan

Msimamizi wa mbuga hiyo Bw Dickson Ritan amemwambia mwandishi wa BBC Paula Odek kwamba ndege hao wamepungua kutokana na ongezeko la maji katika ziwa hilo ambayo yameathiri chakula cha ndege hao, ambao hula chakula chenye chumvi nyingi.

Utafiti wa kisayansi umebaini kwamba vyanzo vya maji ambavyo vinamwaga maji katika ziwa hilo kwa miaka mitano iliyopita, sana mito kutoka msitu wa Mau, vinamwaga maji kwa wingi katika ziwa hilo ambalo halina njia ya kutoa maji nje.

Bw Ritan amesema, kulingana na utafiti uliofanywa hapo awali, kumekuwa na ongezeko la chembechembe za madini ya vyuma vizito katika maji ya ziwa hilo na huenda hilo kwa kiasi fulani limeathiri idadi ya ndege hao.

Image caption Flamingo katika mbuga ya wanyama ya ziwa Nakuru

Eneo la kilomita mbili mraba ambalo awali lilijaa miti na majani sasa limefunikwa na maji kutoka kwenye ziwa. Badala ya mtu kuwaona flamingo eneo hilo kama ilivyokuwa kawaida zamani, sasa taswira inayomkaribisha mtu ni miti iliyokauka ikiwa imesimama kwenye maji kama viashiria vya 'mauti'.

Mwanaharakati wa uhifadhi wa wa mazingira mjini Nakuru, anayepinga matumizi ya karatasi za plastiki, James Wakibia amesema karatasi hizo huchafua mazingiza na hata kuathiri ndege katika ziwa Nakuru.

Image caption Mwanaharakati wa uhifadhi wa mazingira James Wakibia

Bw Wakibia ameongezea kwamba karatasi hizo zina madhara mengi kwa mazingira na amewasihi watu kutozitumia karatasi hizo.

Amekuwa akiendesha kampeni ya kutaka karatasi za plastiki zipigwe marufuku katika jimbo la Nakuru, ambapo mji mkuu wake Nakuru zamani ulifahamika miongoni mwa miji safi zaidi duniani lakini sasa hilo limesalia tu kuwa kumbukumbu.