Simu nyengine ya Galaxy Note 7 yashika moto US

Samsung Galaxy Note 7
Image caption Samsung Galaxy Note 7

Simu ya pili ya Samsung Galaxy Note 7 iliodaiwa kuwa salama na kampuni hiyo imeshika moto nchini Marekani,kulingana na vyombo vya habari.

Samsung ililazimika kutoa simu nyengine mpya ya simu hiyo aina ya smartphone kufuatia malalamishi ya betri zinazolipuka.

Mtu mmoja mjini Kentucky alisema kuwa alishtuka baada ya kuamka na kupata nyumba yake imejaa moshi ,kulingana na vyombo vya habari nchini humo.

Hatua hiyo inajiri baada ya simu nyengine aina ya Note 7 iliokuwa imerekebishwa kushika moto ndani ya ndege ya SouthWest Airlines siku ya Jumatano.

''Simu hiyo ni miongoni mwa zile zilizorekebishwa, kwa hivyo nilidhani ziko salama'',alisema Michael Klering wa Nicholasville,Kentucky.

Aliongezea kwamba simu hiyo haikuwa imewekwa katika chaji wakati iliposhika moto katika nyumba yake siku ya Jumanne.