Wazazi wachunguzwa kwa kifo cha msichana aliyefunga siku 68

Aradhana Samdariya alifunga kwa siku 68 Haki miliki ya picha UMA SUDHIR

Polisi India wanachunguza wazazi wa msichana mwenye umri wa miaka 13 aliyefariki wiki iliyopita baada ya kufunga kwa siku 68 kama ibada.

Police kusini mwa Hyderabad wameimbia BBC wanchunguza iwapo Aradhana Samdariya alilazimishwa kufunga.

Wazazi wake wanasisitiza kuwa alifunga kwa hiari kama inavyotakiwa katika Jainism, mojawapo ya dini za jadi duniani.

Mkasa huo umesababisha mjadala kuhusuibada ya kufunga India.

Ripoti zinasema Aradhana alikunywa maji ya kuchemshwa tu kwa siku 68.

Siku mbili baada ya kusitisha kufunga wiki iliyopita, alifariki.

Wataalamu wanaamini binaadamu anaweza kukaa bila ya chakula kwa hadi miezi miwili.

Msemaji wa polisi amesema kesi imeanzishwa dhidi ya wazazi wa mtoto huyo baada ya shirika la kutetea haki za watoto kuwasilisha malalmiko.

Kufunga kwa hiari?

"Wazazi wake - LaxmiChand na Manshi Samdariya - wameshtakiwa kwa kutekeleza mauaji kwa kupuuza na kwa kukiuka sheria ya watoto," msemaji alisema.

Wazazi hao ambao ni watengenezaji vyombo vya thamani vya mapambo ya mwili, wamekana kuwa walimlazimisha binti yao kufunga.

"Aliomba ruhusa kufunga upvaas. Tulimwambie akatize baada ya siku 51 lakini alikataa. Alifungwa kwa hiari, hakuna aliyemlazimisha," Bwana Samdariya alisema.

Lakini wanaharakati wa kijamii wamepinga tuhuma ya wazazi hao.

Kifo cha msichana huyo kwa mara nyengine kimeangazia kuhusu ibada na tamaduni kama hizo.

Kufunga ni kawaida kwa baadhi ya dini - Waislamu hufunga kula na kunywa kuanzia jua linapopaa mpaka linapotuwa wakati wa mwezi wa Ramadhani, Wakristo hufunga wakati wa Lent, Wayahudi hufunga kula wakati wa Yom Kippur na Wahindu hufunga wakati wa shughuli mbalimbali za kidini.

Lakini dini zote hazikubali kufunga kiasi cha mtu kufa na njaa.

Hatahivyo, viongozi wa dini ya Jain wametetea kufunga kwa muda mrefu.