Mshukiwa wa ugaidi Al-Bakr azuiwa na polisi Ujerumani

Jaber al-Bakr Haki miliki ya picha AFP/Getty Images

Baada ya kusakwa kwa siku mbili, Polisi Ujerumani imemkamata raia wa Syria anayeaminika kupanga shambulio la kijihadi.

Jaber al-Bakr, aliyewasili Ujerumani kama mkimbizi, alikamatwa kwenye nyumba moja mjini Leipzig Jumatatu alfajiri.

Aliomba usaidizi kutoka kwa raia mwengine wa Syria, aliyewaarifu polisi na kumfunga kwa kamba, taarifa zinasema.

Al-Bakr alianza kusakwa baada ya polisi kugundua vilipuzi katika nyumba aliyokuwa akiishi .

Katika uvamizi wa awali mjini Chemnitz mapema Jumamosi, al-Bakr, mwenye umri wa miaka 22, aliponyoka kukamatwa wakati maafisa walipofyetua risasi katika jaribio lililotibuka la kumkamata.

'Maabara ya vilipuzi'

Polisi iligunduwa vilipuzi na kilo ya kemikali katika nyumbani yake kwenye mji wa mashariki Chemnitz. Taarifa zinaashiria kemikali hiyo ni TATP, kemikali ya vilipuzi iliyotumiwa katika mashambulio ya kijihadi Paris na Brussels katika mwaka uliopita.

Duru za usalama zilitaja nyumba ya al-Bakr's kama 'maabara ya vilipuzi' na waliviharibu vilipuzi hivyo katika mlipuko uliodhibitiwa.

Haki miliki ya picha EPA
Image caption Polisi walivamia nyumba hii Leipzig Jumatatu alfajiri
Haki miliki ya picha AFP
Image caption Robot ya kuharibu mabomu ilitumwa katika kitu cha treni cha Chemnitz

Maafisa nchini wamehofia huenda kuna mpango wa kulenga uwanja wa ndege Berlin.

Jumapili usiku Polisi walidokezwa na raia mwengine wa Syria anayeishi Leipzig ambaye Jaber al-Bakr aliwasiliana naye kutoka kituo kikuu cha usafiri cha mji huo.

Jumatatu asubuhi, polisi ilifululiza ndani ya nyumba iliopo katika mtaa wa Paunsdorf mjini humo na kumpata mshukiwa amefungwa kwa kamba, mtandao wa Spiegel Ujerumani unaripoti.

Jaber Al-Bakr aliwasili Ujerumani Februari 2015 na alipewa hifadhi rasmi November, vyombo vya habari Ujerumani vinasema.

Anasemkana kuwa na ushirikiano na kundi la Islamic State. Antarajiwa kusafirishwa hadi mjini Karlsruhe baadaye Jumatatu.

Zaidi ya wahamiaji milioni moja waliwasili Ujerumani mwaka jana, wengi wanaotoroka mzozo wa Syria.