Syria: Ufaransa yataka Urusi ishtakiwe ICC kwa uhalifu wa kivita

Bustan al-Basha, Aleppo Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Urusi ilitumia kura batili kuzuia azimio la Umoja wa Mataifa la kutaka kushitishwa kwa uangushaji mabomu

Rais wa Ufaransa Francois Hollande amependekeza kwamba Urusi inafaa kushtakiwa kwa uhalifu wa kivita kutokana na mashambulio ya mabomu yanayotekelezwa na ndege za kivita za taifa hilo Aleppo, Syria.

Bw Hollande ameambia runinga moja ya Ufaransa kwamba taifa hilo linafaa kushtakiwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC).

Amedokeza pia kwamba huenda akakataa kukutana na Rais wa Urusi Vladimir Putin, ambaye atazuru Ufaransa wiki ijayo.

"Hawa ni watu ambao ni waathiriwa wa uhalifu wa kivita. Wanaotenda haya wanafaa kuwajibishwa, hata kama ni katika mahakama ya ICC," Bw Hollande aliambia TMC.

"Ikitokea kwamba nikutane naye (Bw Putin) nitamwambia kwamba haikubalini. Hili linaweza pia kuathiri sana sifa za Urusi."

Wiki iliyopita, Urusi ilitumia kura batili kupinga azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa la kutaka kusitishwa kwa urushaji mabomu Aleppo.

Azimio hilo lilikuwa limewasilishwa na Ufaransa na Uhispania.

Moscow imekanusha madai kwamba inashambulia raia na badala yake imekuwa ikisisitiza kwamba inawashambulia magaidi.

Urusi na Syria si wanachama wa ICC.