Coleen Rooney ashutumu wanaomkosoa Wayne

Coleen Rooney Haki miliki ya picha Getty Images

Coleen Rooney, mke wa nahodha wa Manchester United na England Wayne Rooney, amewashutumu wanaomkosea mumewe akisema sasa wamezidi.

Amewataka "kufyata ndimi zao" na kusema kwamba wao ni binadamu hawajaungwa kwa plastiki.

"Sisi hatujaundwa kwa plastiki, yeye si wa plastiki, sisi ni binadamu," amesema.

Nahodha huyo wa England alizomewa na mashabiki mechi ambayo England walilaza Malta Jumamosi.

Amewekwa kwenye benchi mechi ya kufuzu kwa Kombe la Dunia itakayochezwa Jumanne dhidi ya Slovenia.

Mashabiki wengi sasa wanasema huenda muda umefika kwa Rooney kustaafu soka ya kimataifa.

Lakini Coleen amekerwa nao na kusema: "Nipanda sana vile kila mtu ana maoni yake. Tulieni, twacheni. Baadhi wanasahau kwamba watu wengine wana hisia pia."

Lakini wengine wanasema wana haki ya kuzungumzia uchezaji wa Rooney kwa sababu analipwa pesa nyingi.

Haki miliki ya picha Getty Images

Coleen amesema ukosoaji ambao umeelekezwa kwa mumewe unawaathiri watoto wao pia.

Wayne Rooney alichezea taifa lake mechi ya 117 dhidi ya Malta. Amefunga bao moja pekee katika mechi 12 za majuzi zaidi alizochezea taifa lake na klabu yake msimu huu.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Gareth Southgate, kaimu meneja wa England amesema haikuwa haki mashabiki kumzomea Rooney