Putin afuta ziara nchini Ufaransa

Rais Putin alitarajiwa kufanya ziara nchini Ufaransa baadaye mwezi huu Haki miliki ya picha AFP/GETTY IMAGES
Image caption Rais Putin alitarajiwa kufanya ziara nchini Ufaransa baadaye mwezi huu

Rais wa Urusi Vladimir Putin amefuta ziara yake nchini Ufaransa wakati unaendelea kushuhudiwa mzozo kuhusu Syria.

Alitarajiwa kukutana na Rais wa Ufaransa Francois Hollande na kufungua kaniss jipya la Orthodox baadaye mwezi huu.

Lakini baada ya serikali ya Ufaransa kusema kuwa mazungumzo yataegemea zaidi suala la Syria ziara hiyo ilifutwa.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Ufaransa ina wasi wasi na mashumbulio yanayoungwa mkono na Urusi mjini Aleppo

Siku ya Jumatatu Hollande alipendekeza kwamba Urusi inafaa kushtakiwa kwa uhalifu wa kivita kutokana na mashambulio ya mabomu yanayotekelezwa na ndege za kivita za Urusi mjini Aleppo, Syria.

Bwana Hollande aliiambia runinga moja ya Ufaransa kwamba taifa hilo linafaa kushtakiwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC).

Alidokeza pia kwamba huenda angekataa kukutana na Rais wa Urusi Vladimir Putin, wakati wa ziara hiyo

"Hawa ni watu ambao ni waathiriwa wa uhalifu wa kivita. Wanaotenda haya wanafaa kuwajibishwa, hata kama ni katika mahakama ya ICC," Bw Hollande aliambia TMC.

Image caption Urusi imekanusha madai kwamba inashambulia raia na badala yake imekuwa ikisisitiza kwamba inawashambulia magaidi.

Wiki iliyopita, Urusi ilitumia kura ya turufu kupinga azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa la kutaka kusitishwa kwa urushaji mabomu Aleppo.

Azimio hilo lilikuwa limewasilishwa na Ufaransa na Uhispania.

Urusi imekanusha madai kwamba inashambulia raia na badala yake imekuwa ikisisitiza kwamba inawashambulia magaidi.

Urusi na Syria si wanachama wa ICC.