Marekani yashambulia waasi wa Houthi nchini Yemen

Manowari ya USS Mason Haki miliki ya picha AP
Image caption Manowari ya USS Mason imeshambuliwa mara mbili

Jeshi la Marekani limtekeleza mashambulizi dhidi ya mitambo ya rada ya waasi nchini Yemen baada ya manowari ya Marekani kushambuliwa kwa mara ya pili katika kipindi cha siku chache.

Manowari hiyo ya Marekani ilishambuliwa ikiwa maeneo ya bahari ya kimataifa.

Pentagon imesema tathmini ya awali inaonesha maeneo matatu yenye mitambo ya rada, ambayo yanashukiwa kutumiwa kutekeleza mashambulio hayo, yameharibiwa.

Jeshi hilo la Marekani limesema maeneo yaliyoshambuliwa yanamilikiwa na waasi wa Houthi wanaoungwa mkono na Iran.

Pentagon imesema mashambulio hayo ya makombora yaliidhinishwa na Rais Obama, na yalitekelezwa kulinda manowari za Marekani na wanajeshi wake na pia kuhakikisha uhuru wa watu wanaopitia Bahari ya Sham kwenye ufuo wa Yemen.

Mashambulio hayo yalitekelezwa kwa makombora ya Tomahawk yaliyofyatuliwa kutoka kwa manowari ya USS Nitze.