Shinikizo kuidhinisha mahakama maalum kwa maovu ya S.Kusini

Rais Salva Kiir na aliyekuwa makamu wake Riek Machar

Amnesty International limeishutumu jumuiya ya kimataifa kwa kujiburura katika kuidhinisha mahakama maalum kusikiza kesi zinazotuhumiwa Sudan kusini za uhalifu wa kivita.

Inafuata kuongezeka kushuhudiwa ghasia katika miezi ya hivi karibuni na wasiwasi unoaongezeka katika mji mkuu Juba, licha ya kuidhinishwa makubaliano ya amani mwaka jana.

Shirika hilo la kimataifa la kutetea haki za binaadamu, linasema ahadi inayoungwa mkono na waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry na viongozi wengine wa kieneo pamoja na pande mbili za mzozo kuidhinisha mahakama maalum, imekwama.

Linasema ukiukaji wa sasa uliosababisha maelfu kuuawa, wanawake kubakwa, na vijiji kuharibiwa ni mambo yanayopasa kutoa shinikizo jipya katika kufanikisha kuundwa mahakama hiyo maalum.

Image caption Maelfu wameyatoroka makaazi yao Sudan Kusini

Takriban miaka mitatu baada ya kuzuka ghasia katika taifa jipya Afrika, zilizowalazimisha watu milioni 2.6 kuyatoroka makaazi yao, na kusabaisha vifo vya maelfu huku wengine wakijeruhiwa, Amnesty International linaonya kuwa ahadi ya kuidhinishwa mahakama hiyo maalum imepuuzwa.

Makubaliano ya amani yalioitiwa saini mwaka jana kati ya rais Salva Kiir na aliyekuwa makamu wake, Riek Machar yalitoa ahadi ya kuidhinisha mahakama maalum kusikiza tuhuma za uhalifu wa kivita ikiwemo mauaji na ubakaji.

Wakati Sudan kusini sio mwanachama wa mahakama ya kimataifa ya jinai ICC, pendekezo ilikuwa ni kuunda mahakama hiyo itakayojumuisha mahakimu wa nchini na wa kimataifa ambayo iwapo itabidi, makaazi yake yatakuwa nje ya nchi ya Sudan Kusini.

Kundi hilo la kutetea haki za binaadamu linasema maovu yanayotuhumiwa ambayo Muungano wa Afrika tayari imenukuu 'ni lazima haki itetendeka' na kusema mahakama hiyo haitoshughulikia ukiukaji wa haki za binaadamu lakini pia ni muhimu katika 'nguzo ya kufikia amani ya kudumu'.

Amnesty linasema kesi ya hivi karibuni dhidi ya aliyekuwa rais wa Chad, Hissene Habre kwa uhalifu wa kivita, iliyosikizwa katika mahakama ya Afrika, inapaswa kuwa kama kichochezi cha kuwawajibisha viongozi wa Sudan kusini.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii