Clinton na Trump: Nani anaongoza?

Donald Trump and Hillary Clinton

Wamarekani watapiga kura tarehe 8 Novemba kumchagua rais atakayemrithi Barack Obama wa chama cha Democratic.

Hapa tutakupatia tathmini ya udadisi wa kura za maoni nchini humo, hasa kuhusu ushindani kati ya mgombea wa Democratic Hillary Clinton na mwenzake wa Republican Donald Trump.

Tunafahamu nini kutokana na kura za mapema?

Upigaji wa kura mapema umekuwa ukifanyika katika majimbo mengi nchini Marekani na kufikia sasa inakadiriwa kwamba Wamarekani 46 milioni tayari wamepiga kura.

Ingawa kura hizi zitahesabiwa baada ya vituo kufungwa Jumanne, baadhi ya majimbo huta takwimu na maelezo kuhusu waliopiga kura kwa mfano kuhusu idadi ya waliopiga kura na iwapo wamejiandikisha kuwa wa chama cha Republican au Democratic.

Jimbo la Nevada, kwa mfano, tunajua kwamba karibu watu 800,000 walipiga kura kabla ya kufungwa kwa upigaji wa kura za mapema tarehe 4 Novemba.

Asilimia 42 walikuwa wanachama wa Democratic na 36% wanachama wa Republican. Takwimu hizo hazina tofauti kubwa na hali 2012, ambapo Barack Obama aliongoza kwa 6.7%.

Bila shaka, hakuna sheria yoyote inayosema kwamba mwanachama wa chama fulani lazima ampigie kura mgombea wa chama hicho, hasa ikizingatiwa kwamba Bw Trump na Bi Clinton wamekuwa wakitoa wito kwa wanachama wa vyama pinzani ambao wametamaushwa na wagombea wa vyama hivyo kuwaunga mkono.

Lakini takwimu hizo kutoka Nevada kidogo zinashangaza ikizingatiwa kwamba kura za maoni za karibuni zimeonesha Bw Donald Trump anaongoza jimbo hilo.

Hilo halina maana kwamba matokeo hayo ya kura za maoni si sahihi, wanaomuunga mkono Bw Trump huenda wanasubiri kujitokeza siku ya uchaguzi.

Lakini labda wanaofanya kura za maoni huenda wamekosea, labda iwe kwamba wanashindwa kuzingatia kikamilifu kujitokeza kwa wingi kwa wapiga kura wa asili ya Hispania (Mexico/Latino). Hilo limeshuhudiwa katika majimbo kadha mengine, yakiwemo Arizona, Colorado, Florida na Carolina Kaskazini, kwa mujibu wa utathmini kutoka kwa Catalist, kampuni ya data inayofanya kazi kwa ushirikiano na maafisa wa kampeni wa Bi Clinton.

Katika uchaguzi wa awali, haikuwa wazi wapiga kura wa asili ya Hispania wangeunga mkono nani (George W Bush wa Republican alishinda 40% ya kura zao 2004), lakini mwaka huu imekuwa wazi kiasi kutokana na msimamo mkali wa Bw Trump dhidi ya Wahamiaji na watu kutoka Mexico. Kundi la utafiti la Latino Decisions linakadiria kwamba 79% ya wapiga kura wa asili ya Hispania watamuunga mkono Bi Hillary Clinton.

Jambo ambalo tunafahamu wazi ni kwamba watu wengi zaidi walipiga kura mapema mwaka huu ukilinganisha na zamani. Mwaka 2012, waliopiga kura mapema walikuwa 32 milioni pekee. Zaidi ya watu 40 milioni wamepiga kura mapema mwaka huu.

Maelezo ya picha,

Utathmini wa kura za maoni kufikia 8 Novemba, 2016.

Habari ambazo si njema kwa Hillary Clinton ni kwamba uongozi wake kwenye kura za maoni ulianza kupungua kitaifa na katika baadhi ya majimbo yanayoshindaniwa kabla ya mkuu wa FBI James Comey kutangaza kuanzishwa kwa uchunguzi mpya kuhusu barua pepe zake 28 Oktoba.

Kura ya maoni ya ABC News/Washington Post kwa mfano ilionesha Bi Clinton alikuwa mbele ya Donald Trump kwa asilimia 12 mnamo 23 Oktoba lakini uongozi huo ulikuwa umepungua na kufikia asilimia moja wiki moja baadaye.

Msisimko wa watu kumpigia Bi Clinton kura ulikuwa pia umeshuka kiasi, wale waliosema wana hamu sana kumpigia kura wakishuka kutoka 51% hadi 47%.

Matokeo ya kura za maoni kawaida hukaribiana sana uchaguzi unapokaribia lakini sasa inaonekana habari za uchunguzi wa FBI ziliathiri matokeo.

Bw Comey alitangaza 6 Novemba kwamba hakuna ushahidi uliopatikana, lakini huenda madhara yalikuwa tayari yamefanyika.

Hata hivyo, kura za maoni zimeanza kuashiria kwamba Bi Clinton anaimarika.

Kura za maoni zina umuhimu?

Ni vigumu kubaini maoni ya watu zaidi ya 300 milioni lakini watafiti wa maoni bado hujaribu. Watu wanaotumiwa huwa ni 1,000 hivi na kwa kuzingatia maadili ya utafiti na sayansi, huwezekana kubashiri matokeo.

Majimbo yanayoshindaniwa sana?

Kuna majimbo 13 ambayo yanatarajiwa kushindaniwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu. Hapa chini ni ramani ya majimbo hayo na uwezekano wa nani atashinda kwa kutumia matokeo ya kura ya maoni ya tovuti ya Real Clear Politics.

Ndipo Donald Trump aweze kupata nafasi nzuri, anahitaji kujishindia Florida na Ohio na majimbo mengine kadha. Kwa sasa hali ilivyo, Clinton yupo mbele kidogo Florida na Ohio.

Matokeo kamili ya kura za maoni za karibu majimbo hayo yanayoshindaniwa ni kama ilivyo hapa chini.

Trump na Clinton ndio wagombea pekee?

La hasha, kuna wagombea wengine wengi. Lakini wale wakuu ni Hillary Clinton na Donald Trump.

Mgombea wa Green Party Jill Stein, 66, ni daktari na mwanaharakati ambaye anatarajia kupata uungwaji mkono kutoka kwa wafuasi wa Democratic waliomuunga mkono Bernie Sanders ambao bado wanampinga Bi Clinton.

Gavana wa zamani wa New Mexico Gary Johnson, 63, anawania kupitia chama cha Libertarian Party na sana anaangazia kuwavutia wafuasi wa Republican wasiopendezwa na Bw Trump.

Kwa mujibu wa Real Clear Politics, Bi Stein ana karibu 2% ya kura naye Bw Johnson ana zaidi ya 7%.

Wawili hawa wanaweza kuchangia sana kuamua mshindi kwani watavutia wapiga kura kutoka kwa wagombea wakuu.

Clinton amefanya vyema?

Bi Hillary Clinton amepigiwa upatu kushinda lakini kuna wakati mwingine ambapo uongozi wake hupunguzwa sana. Majuzi zaidi ilikuwa mapema Septemba. Mwanzo, alionekana kuwakosoa wafuasi wa Donald Trump na kusema ni "kapu la watu wa kusikitisha" na wasioweza kuokolewa.

Baadaye, alionekana kukaribia kuzirai wakati wa sherehe ya ukumbusho wa shambulio la 9/11.

Umaarufu wake ulishuka kidogo lakini baadaye akajikwamua.

Trump aliongoza lini mwisho?

Wakati mmoja Trump aliachwa nyuma sana na Bi Clinton, akiwa nyuma kwa karibu 20% majira ya joto 2015 wagombea walipokuwa wengi. Hata hivyo, amefanikiwa kumpita Bi Clinton mara chache sana.

Mwisho ni alipopokea idhini ya kuwania urais mwisho wa Julai kwenye Kongamano la Taifa la Republican.

Hakuongoza kwa muda mrefu kwani mpinzani wake naye alijikwamua kongamano la Democratic lilipofanyika siku chache baadaye.

Wagombea wenza walisaidia?

Zamani wagombea wenza walisaidia sana, mfano Bill Clinton alipanda 12% baada ya kumteua Al Gore mgombea mwenza 1992.

Lakini karibuni mambo yamekuwa tofauti na mwaka 2016 hakujakuwa na mabadiliko makubwa.

Mgombea mwenza wa Trump, Gavana wa Indiana Mike Pence aliteuliwa Julai 15 naye wa Clinton, gavana wa zamani wa Virginia Tim Kaine akatangazwa Julai 22, lakini hakukutokea mabadiliko makubwa kwenye kura za maoni.