Mshukiwa wa ugaidi wa Tanzania apata tatizo la akili Kenya

Shambulio la Chuo Kikuu cha Garissa nchini Kenya Haki miliki ya picha EPA
Image caption Shambulio la Chuo Kikuu cha Garissa nchini Kenya

Raia wa Tanzania aliyeshtakiwa kwa kuhusika katika shambulio la kigaidi la chuo kikuu cha Garissa 2015 ambapo takriban watu 149 waliuawa amepata ugonjwa wa kiakili akiwa jela.

Kulingana na gazeti la Daily Nation nchini Kenya, Rashid Charles Mberesero aligunduliwa kuwa hawezi kuendelea na kesi baada ya ripoti ya daktari wa maswala ya kiakili kusema kuwa amekuwa akitibiwa tatizo la kuwa na ''mienendo isiyo eleweka'' katika jela ya kamiti.

Gazeti hilo linasema kuwa ameshtakiwa pamoja na Mohamed Ali Abdikar, Hassan Aden Hassan, Sahel Diriye na Osman Abdi.

Wamekana mashtaka 162 ya ugaidi.

Kulingana na Daily Nation, siku ya Jumatano, upande wa mashtaka ulitaka kupewa muda kujadiliana jinsi ya kuendelea na kesi hiyo dhidi ya wenzake kutoka Kenya.

Matokeo ya ripoti ya ukaguzi wa akili iliowasilishwa katika mahakama ilisema kuwa alidungwa sindano yake ya kila mwezi mnamo tarehe 12 mwezi Septemba.

''Amekuwa akikabiliwa na matatizo yasio ya kawaida, ambapo anaamini watu wote karibu naye wana nia za kishetani'', daktari Mucheru Wang'ombe aliandika katika ripoti hiyo.

Kulingana na Daily Nation, daktari huyo amesema kuwa mshukiwa huyo anahitaji matibabu na uchunguzi wa kila mara wa akili yake.

''Ripoti hiyo inasema kuwa mshukiwa huyo apewe matibabu katika hospitali ya Mathare kila mwezi na hayuko katika hali ya kuweza kuendelea na kesi hiyo na kwamba majadiliano yanaendelea'', alisema kiongozi wa mashtaka Eddie Kadebe.