Ushahidi wa ushawishi wa washirika wa Zuma kutolewa

Rais Jacob Zuma
Image caption Rais Jacob Zuma

Saa chache kabla ya kuondoka mamlakani kwa afisa mkuu wa tume ya kukabiliana na ufisadi nchini Afrika Kusini Thudi Madonsela, BBC imebaini kwamba ushahidi wa simu aliopata ni muhimu katika ripoti ya uchunguzi wake ambao rais Jacob Zuma anajaribu kuukandamiza.

Duru zilizo karibu na bi Madonsela zinasema kuwa ushahidi uliokusanywa kutoka kwa simu, unaonyesha kwamba mtu aliyeteuliwa kumrithi waziri wa fedha aliye maarufu ambaye alifutwa kazi kwa kishindo kikubwa mwaka uliopita alikuwa amezuru katika nyumba ya familia ya Gupta, ambayo inadaiwa kuwa na ushawishi mkubwa kwa rais.

Wakosoaji wa afisa huyo wa kukabiliana na ufisadi wanasema amezidisha uwezo wake na yuko katika harakati za kutaka kumuangusha rais Zuma, lakini amesisitiza kuwa anafanya kazi yake.

Duru zinasema kuwa ushahidi huo wa simu unaenda sambamba na taarifa mfichuzi mmoja anayesema kuwa famili ya Gupta ina ushawishi mkubwa katika uteuzi wa nyadhfa mbalimbali serikalini.

Image caption Bi Madonsela

Simu hizo zinadaiwa kufichua kwamba usiku kabla ya waziri wa fedha Nhlanla Nene kufutwa kazi mnamo mwezi Disemba,mtu aliyechaguliwa kuchukua mahala pake alikunywa chai na familia ya Gupta nyumbani kwao huko Johannesburg.

Bi Madonsela alikuwa amepanga kutoa ripoti yake,saa kadhaa kabla ya kuondoka madarakani,baadaye leo,lakini amezuia kisheria na rais.

Chama tawala cha ANC kimesema kuwa kinaunga mkono kutolewa kwa ripoti kuhusu ushawishi wa kisiasa walio nao washiriki wa rais Zuma.