Mexico kumkabidhi El Chapo kwa maafisa Marekani

Joaquin "El Chapo"

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha,

Guzman alikuwa mkuu wa genge la walanguzi la Sinaloa

Mexico inapanga kumkabidhi mlanguzi hatari wa mihadarati Joaquin "El Chapo" Guzman kwa maafisa wa Marekani mwezi Februari, kwa mujibu wa afisa mmoja mkuu nchini Mexico

Hata hivyo, Guzman anaweza akakata rufaa uamuzi wa kumpeleka Marekani na mawakili wake wanasema watapigana vita hadi mwisho.

Anakabiliwa na mashtaka kadha nchini Marekani yakiwemo ulanguzi wa dawa na mauaji.

Kiongozi huyo wa genge la Sinaloa anazuiliwa katika gereza la Ciudad Juarez, karibu na mpaka wa Mexico na Marekani, chini ya ulinzi mkali.

Alikamatwa mwezi Januari miezi sita baada yake kutoroka gerezani kwa kupitia njia ya chini ya ardhi iliyochimbwa hadi kwenye seli yake gerezani.

Alikuwa tayari ametoroka kutoka gereza la ulinzi mkali mara moja awali, na akakaa miaka 13 akitafutwa sana na maafisa wa usalama.

Kamishna mkuu wa usalama wa Mexico Renato Sales Heredia amesema kwenye mahojiano na kituo kimoja cha runinga kwamba Mexico inatarajia kumhamishia Marekani mshukiwa huyo "Januari au Februari".

Lakini wakili Jose Refugio Rodriguez, amesema kuna kesi nyingi za rufaa ambazo uamuzi wake unasubiriwa na kwamba hilo haliwezi kufanyika haraka.

"Muda huo hautoshi," Bw Rodriguez amesema na kudokeza kwamba njia pekee ya kumpeleka Guzman Marekani mapema mwaka ujao ni kwa kutumia nguvu pekee.