Bei ya mafuta: Amir wa Kuwait avunja bunge

Mgogoro wa bei ya mafuta wasababisha bunge la kuwait kuvunjwa
Image caption Mgogoro wa bei ya mafuta wasababisha bunge la kuwait kuvunjwa

Baraza la mawaziri la Kuwait limejiuzulu huku bunge likivunjwa na hivyobasi kuitisha uchaguzi mpya.

Hatua hiyo inafuatia mgogoro kati ya wabunge na serikali kufuatia kupandishwa kwa bei ya mafuta katika taifa hilo lenye utajiri mkubwa wa mafuta.

Runinga ya taifa imesema kuwa ukosefu wa ushirikiano ndio sababu ya tukio hilo.

Huku bei ya mafuta kote duniani ikisalia kuwa ya chini ,serikali ya Kuwait imepunguza baadhi ya faida ikiwemo ruzuku ya mafuta na kupandishwa kwa bei ya petroli hadi asilimia 80.

Hili lilizua pingamizi.Serikali ilitarajiwa kumaliza muda wake wa miaka minne ifikiapo Julai mwaka ujao.

Wabunge katika bunge la sasa wanadhaniwa kuunga mkono serikali lakini wamewasilisha maombi matatu ya kuwahoji mawaziri kuhusu bei hizo mpya.

Baada ya mkutano wa dharura uliotishwa na serikali siku ya Jumapili jioni,Amir wa Kuwait Sheikh Sabah al-Ahmad al Sabah,alitoa amri ya kulivunja bunge kutokana na hali ilivyo katika eneo hilo.

Runinga ya taifa ilitangaza kuwa mawaziri wote wamejiuzulu.