Mfahamu, Kigeli V Ndahindurwa, mfalme wa mwisho wa Rwanda

Mfalme Kigeli V Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Mfalme Kigeli V alikuwa na miaka 23 alipotawazwa

Kwa miaka mingi, Rwanda ilitawaliwa na wafalme ambao walifahamika kwa jina Mwami/Umwami, kwa wingi wakiitwa Abami.

Mwami wa mwisho kutawala Rwanda alikuwa Mfalme Kigeli V (Kigeli wa Tano) ambaye aliondolewa madarakani 1961.

Mfalme huyu, ambaye amekuwa akiishi uhamishoni nchini Marekani, amefariki dunia.

Mfalme Kigeli V alizaliwa tarehe 29 Juni, 1936 eneo la Kamembe kusini magharibi mwa Rwanda akiwa mwana wa Mfalme Yuhi V Musinga, na Malkia Mukashema. Alitoka jamii ya Watutsi.

Wakati wa kuzaliwa kwake, babake alikuwa ameondolewa madarakani na Wabelgiji kwa kushukiwa kupendelea sana wakoloni wa awali Ujerumani.

Alikuwa amewekwa eneo lililotengwa kusini magharibi mwa Rwanda lakini miaka minne baadaye, familia yao yote ilihamishiwa Congo. Babake alifariki kutokana na kichomi (nimonia) mwaka 1944.

Jina lake la kuzaliwa ni Ndahindurwa. Alibatizwa katika kanisa Katoliki la Kirumi na akaongezewa jina Jean-Baptiste.

Alipata masomo ya msingi katika shule za Groupe Scolaire d'Astrida kisha akapata elimu ya juu katika chuo cha Nyangezi katika nchi ya Zaire, ambayo kwa sasa hufahamika kama Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Baada ya kuondolewa madarakani kwa babake Mfalme Yuhi V Musinga, kakake wa kambo alitawazwa Mfalme Mutara III Rudahigwa. Alisaidia kutetea familia ya Musinga kukubaliwa kurejea nyumbani Rwanda.

Mfalme Kigeli baada ya kumaliza masomo yake alifanyia kazi utawala wa wakoloni wa Ubelgiji katika jimbo la Astrida kusini mwa Rwanda kati ya 1956 na 1958.

Aliteuliwa naibu chifu wa eneo la Bufundu mwaka 1959, na baadaye akateuliwa kuwa chifu kamili.

Mfalme Mutara aliugua baada ya kudungwa sindano na daktari Mbelgiji na akafariki dunia Julai 25, 1959.

Mutara alikuwa ameoa lakini hakuwa amejaliwa watoto. Wakati wa mazishi yake, wasimamizi wa urithi walimtangaza Ndahindurwa kuwa mfalme mpya na akachukua jina Mfalme Kigeli V, wakati huo akiwa na miaka 23 pekee.

Novemba mwaka huo, chini ya mwezi mmoja baada yake kuapishwa, Wahutu walio wengi waliasi na kuwaua mamia ya Watutsi huku wengine wakilazimika kukimbilia nchi jirani.

Wahutu walimtazama Mfalme Kigeli kama mwakilishi wa "mfumo dhalimu wa wakoloni na Watutsi".

Huwezi kusikiliza tena
Mwafalme wa mwisho wa Rwanda, Kigeli V, afariki dunia

Mfalme Kigeli V alikimbilia Congo, ambayo ilikuwa imejipatia uhuru siku chache awali.

Alirejea kwa muda mfupi Septemba mwaka uliofuata wakati kura ilikuwa inapigwa kuamua hatima ya taifa hilo. Zaidi ya asilimia 80 walipiga kura kupinga utawala wa kifalme na kumpinga Mfalme Kigeli, wakati huo akiwa chini ya kizuizi cha nyumbani.

Tarehe 2 Oktoba, 1961, siku chache kabla ya uchaguzi mkuu na miezi michache kabla ya Rwanda kujipatia uhuru wake, Mfalme Kigeli alisafirishwa hadi Tanzania kuishi uhamishoni.

Hakuwahi kurejea tena nchini Rwanda tangu siku hiyo. Rwanda ilijipatia uhuru kama Jamhuri, Mhutu Dominique Mbonyumutwa akiwa rais.

Kwa miaka iliyofuata, aliishi katika nchi kadhaa uhamishoni.

Alikuwa amepewa nyumba na Idi Amin nchini Uganda mwaka 1973 lakini mtawala huyo wa kiimla alipoondolewa madarakani miaka sita baadaye, akalazimika kuikimbia nchi hiyo na kuingia Kenya.

Miaka ya 1980, hali ya kisiasa nchini Rwanda ilianza kuwa mbaya na Rais Juvenal Habyarimana aliyekuwa ametawala kwa mabavu kwa miongo miwili alilazimishwa kugawana madaraka na vyama vingine. Makundi ya Watutsi yaliyokuwa uhamishoni yalianza uvamizi na hapo uhasama baina ya Wahutu na Watutsi ukafufuliwa.

Rais Habyarimana alikuwa rafiki ya Rais wa Kenya Daniel arap Moi na Mfalme Kigeli hakujihisi salama na ndipo akatumia urafiki aliokuwa ameunda na Mmarekani Bill Fisher kuhamia Marekani.

Alitua Oklahoma mwaka 1992.

Kwenye mahojiano na BBC mwaka 2007, Mfalme Kigeli alisema alitaka kurejea nchini mwake na kutawala tena.

Hata hivyo, alisema angerejea tu iwapo Wanyarwanda walimtaka arejee na iwapo wangekuwa tayari kumtambua kama mfalme wa kikatiba.

Alisema alikuwa amekutaka na Rais Kagame na wakajadiliana kuhusu hilo.

Mambo muhimu

  • Alizaliwa 29 Juni 1936 kusini mwa Rwanda
  • Jina lake kamili ni Ndahindurwa Jean-Baptiste
  • Alikuwa wa jamii ya Tutsi
  • Aliwahi kuishi uhamishoni Tanzania, Uganda na Kenya
  • Alihamia Marekani 1992
  • Amefariki akiwa na umri wa miaka 80

Mfalme Kigeli alisema Rais Kagame aliahidi kwenda kushauriana na serikali yake kuhusu hilo.

Alikuwa bado anajichukulia kama mfalme kwa sababu alisema aliondolewa uongozini kwa njia isiyo halali.

"Raia wa Rwanda wanaweza kunitaka au huenda wasinitake. Lakini ndipo nirejee nyumbani, nahitaji kufahamu iwapo bado wanataka niwe mfalme wao," aliambia BBC.

Haki miliki ya picha AFP/Getty Images
Image caption Mfalme Kigeli V Ndahindurwa alitaka kurejea Rwanda

Makala kwenye tovuti ya Washingtonian.com inasema aliishi maisha ya ufukara uhamishoni Marekani.

Hata hivyo, Mfalme Kigeli aliambia mwandishi wa makala hiyo kwamba: "Huwa wananiita Mfalme wa Afrika."

Aidha, alikuwa na wakfu wa kuwasaidia watoto mayatima na wasiojiweza kutoka Rwanda.

Kwenye tangazo la kifo chake, tovuti ya mfalme huyo taarifa imesema mrithi wa Mfalme Kigeli atatangazwa karibuni.