Rwanda yasikitishwa na kifo cha mfalme Kigeli

Kigeli V Ndahindurwa Haki miliki ya picha AFP/Getty Images
Image caption Mfalme Kigeli V Ndahindurwa alifariki dunia akiwa na miaka 80

Serikali ya Rwanda imetangaza kusikitishwa na kifo cha Mfalme wa mwisho wa nchi hiyo Kigeli V Ndahindurwa aliyefariki Jumapili nchini Marekani.

Rwanda inasema haijapata taarifa zozote kutoka kwa familia ya Mfalme huyo kuhusu mipango ya mazishi lakini kwamba iko tayari kutoa msaada wowote utakaohitajika.

Tangazo fupi lililopakiwa kwenye ukurasa wa Twitter wa ofisi ya msemaji wa serikali, linasema serikali haikupata rasmi taarifa ya kifo cha Mfalme Kigeli Ndahindurwa kutoka kwa familia yake lakini kwamba imesikitishwa na kifo chake.

Tangazo hilo linasema pia kwamba bado haijafahamishwa kuhusu mipango ya mazishi na pahala yatakapofanyika lakini kwamba pindi itakapofahamishwa iko tayari kutoa mchango wowote utakaotakiwa.

Msaidizi wa karibu wa Mfalme Kigeli Boniface Benzige ameiambia BBC kwamba hadi sasa hawajaamua ni wapi na ni lini mwili wa mfalme huyo utazikwa.

"Hatujaafikiana kuhusu mipango ya mazishi yake. Kuna jamaa zake wanaoishi Afrika ambao lazima kwanza wawasili hapa, pia kuna washauri ambao tunashirikiana, hatujaamua la kufanya."

Benzige ameeleza kuwa "bado sina jibu kuhusu hilo"

Amesema Mfalme Kigeli mara kadhaa alionesha nia ya kutaka kurejea nyumbani nchini Rwanda lakini hadi kufikia sasa haijafahamika ikiwa mwili wake utasafirishwa Rwanda.

"Kuhusu hilo Mfalme hakutangaza lolote kuhusu ikiwa atazikwa nchini Rwanda. Mara kadhaa serikali ilimshawishi kurejea lakini yeye alikuwa na masharti yake ili aweze kurejea katika nchi yake na masharti hayo hayakuzingatiwa ndiyo sababu bado alikuwa uhamishoni," ameambia BBC.

Kabla ya kifo chake Mfalme Kigeli alitangaza kwamba bado yeye ni Mfalme wa Rwanda ijapokuwa nchi hiyo inafuata mfumo wa utawala wa jamuhuri.

Alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 80.

Hakuwa na mke wala mtoto lakini wasaidizi wake wanasema wanafikiria kuhusu atakayerithi kiti cha Ufalme.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii