Mahakama DRC yaidhinisha kuahirisha uchaguzi mkuu wa Novemba

Uchaguzi mkuu unazidisha hali ya wasiwasi Congo Haki miliki ya picha AFP

Mahakama ya katiba Katika Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo imeidhinisha ombi lililozusha mzozo la tume ya uchaguzi kuahirisha uchaguzi wa Novemba ili orodha ya usajili wa wapiga kura iwekwe sawa.

Kiongozi wa mahakama ya katiba, Benoit Lwamba Bindu amesema mahakama hiyo inatambua kuwa kuna matatizo ya kiufundi na imeamrisha 'kucheleweshwa kwa sababu zinazoeleweka.'

Imesema tume hiyo ni lazima ichapishe kalenda mpya ya uchaguzi wa urais ambao awali ulipangwa kufanyika Novemba 27.

Tume ya uchaguzi Congo iliwasilisha rufaa mahakamani ya kuchelewesha uchaguzi huo mnamo mwezi September.

Kufikia sasa imesema huenda uchaguzi usiweze kuandaliwa hadi mwishoni mwa mwaka 2018, jambo linalozusha wasiwasi kuwa hofu na ghasia zitaongezeka.

Madaraka na Uongozi

Rais Joseph Kabila alitarajiwa kujiuzulu Desemba baada ya muda wake kikatiba kumalizika baada ya kuhudumu kwa mihula miwili madarakani.

Upinzani unasema kuwa Kabila anajaribu kuendelea kushikilia madaraka kwa kuchelewesha uchaguzi.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Ghasia katika maandamano ya kuipinga serikali ya rais Kabila

Mahakama ya juu imesema, rais Kabila anaweza kusalia madarakani mpaka kiongozi mpya atakapo chaguliwa.

Watu kadhaa wameuawa katika mji mkuu Kinshasa mwezi Septemba baada ya vikosi vya usalama kupambana na maelfu ya waandamanaji wanaoipinga serikali.

Pia siku ya Jumatatu, chama tawala na washirika wengine katika mazungumzo ya kitaifa wamekubaliana kuhusu azimio kuwa uchaguzi wa urais, wabunge na madiwani unapaswa kufanyika April 2018, uamuzi ambao huenda ukapingwa na vyama vikuu vya upinzani nchini, ambavyo vimesusia mazungumzo hayo ya kitaifa.

Vyama vikuu vya upinzani vimetaka jumuiya ya kimataifa na Umoja wa mataifa kuwajibika zaidi na Muungano wa Afrika katika kuidhinisha mazungumzo yalio na hadhi kubwa zaidi na yanayojumuisha pande zote kuhusu kuandaa uchaguzi mkuu, na vimeitisha maandamano ya Oktoba 19 iwapo hakuna hatua itakayo pigwa.

Vimetaka pia tume ya uchaguzi, na mahakama ya kikatiba zifanyiwe mabadiliko, vikieleza kuwa zinampendelea Kabila.

Tangu Congo ijinyakulie uhuru kutoka Ubelgiji mnamo 1960, hapaja shuhudiwa mageuzi ya uongozi kidemokrasia kwa amani.