Hillary Clinton atabahatika mara ya pili?

Bi Hillary Clinton Indianola, Iowa 14 Septemba 2014

Hillary Clinton amehudumu katika nyadhifa nyingi siasa za Marekani, alikuwa mama wa taifa, seneta, waziri wa mambo ya nje. Sasa, anajaribu kwa mara ya pili kutimiza ndoto yake kuu, kuwa rais wa Marekani

Mwanasiasa huyu wa Democtratic wa umri wa miaka 68 alihudumu kama waziri wa mambo ya nje wa Rais Barack Obama mwanzoni mwa utawala wake Januari 2009.

Alijiuzulu muda mfupi baada ya Rais Obama kuchaguliwa tena kwa muhula wa pili.

Ni mwanadiplomasia mashuhuri Marekani na anafahamika sana kwa kusafiri sana nchi mbalimbali na kufuata diplomasia ya kukutana ana kwa ana na wahusika.

Kuzoea kwake kufanya safari nyingi za kuchosha, kunamuandaa vyema kwa changamoto za safari nyingi za kampeni za urais.

Alijaribu mara ya kwanza kuwania urais lakini akashindwa na Rais Obama wakati wa mchujo wa chama cha Democratic mwaka 2008.

Hillary Rodham Clinton

  • Alizaliwa 26 Oktoba, 1947 mjini Chicago
  • Alihitimu kutoka Chuo Kikuu cha Sheria cha Yale, 1973
  • Aliolewa na Bill Clinton mwaka 1975
  • 1993-2001: Alipigania kupanuliwa kwa bima ya afya na haki za wanawake alipokuwa mama wa taifa
  • Alichaguliwa seneta wa New York mwaka 2000
  • Alichaguliwa tena kwa kura nyingi 2006
  • 2008: Alishindwa mchujo wa kuteua mgombea urais chama cha Democratic
  • 2009-2013: Alihudumu kama Waziri wa mambo ya nje

Hillary Diane Rodham alizaliwa Oktoba 1947 mjini Chicago. Miaka ya 1960 alihudhuria masomo Chuo cha Wellesley jimbo la Massachusetts, na akaanza kujihusisha na siasa za wanafunzi.

Alisomea uanasheria katika Chuo Kikuu cha Yale ambapo alikutana na Bill Clinton. Walifunga ndoa 1975. Aliendelea kujihusisha na siasa baada ya Bw Clinton kuwa gavana wa Arkansas mwaka 1978.

Bw Clinton alipokuwa akifanya kampeni za urais mwaka 1992, alisema kwa mzaha kwamba alikuwa anawapa wapiga kura marais wawili "kwa bei ya mmoja".

Kama mke wa rais, Bi Clinto alitetea haki za wanawake na huduma ya afya kwa wote, na hilo likamuongezea sifa nyumbani n ahata nje ya nchi.

Hata hivyo, baada ya kushindwa kufanikisha mpango wa bima ya afya kwa wote, ambao hata haukujadiliwa katika bunge la Congress, wakosoaji wake wengi walimtazama kama mtu mwenye ndoto zisizoweza kutimia na limbukeni kisiasa.

Katikati mwa miaka ya 1990, wakati wa muhula wa pili wa mumewe Bill Clinton, alihusishwa na kashfa kadha zilizoathiri uongozi wake.

Kuliandaliwa vikao vya bunge na uchunguzi ukafanywa kuhusu Kashfa ya Whitewater ', mradi wa ardhi na nyumba ambao familia ya Clinton ilikuwa imewekeza.

Maelezo ya picha,

Hillary Rodham Clinton alipata umaarufu alipokuwa mama wa taifa

Hata hivyo, hawakupatikana na hatia.

Pia aliangaziwa na vyombo vya habari kuhusiana na kashfa za Bw Clinton na wanawake kadha, sana na mkurufunzi aliyefanya kazi White House Monica Lewinsky, ambayo iliangaziwa sana 1998.

Hillary Rodham Clinton alionekana kupata uwezo wa kustahimili mambo makubwa jambo lililomuwezesha kustahimiliki misukosuko katika maisha ya kibinafsi na ya kisiasa.

Aliwashtumu wakosoaji wa mumewe. Alitangaza mwaka 1998, kwenye mahojiano kuhusu kashfa ya Lewinsky, ambayo ilisababisha kuanzishwa kwa vikao vya kutaka kumtoa madarakani Bw Clinton, kwamba kashfa hiyo ilikuwa imeanzishwa na watu wa mrengo wa kulia.

Mwaka 2000, utawala wa Bw Clinton ulipokuwa unakaribia mwisho wake, aliwania wadhifa wa useneta jimbo la New York, na kujiweka katikati katika siasa za chama cha Democratic.

Aliunga mkono kuvamiwa kwa Iraq mwaka 2003 lakini akajitenga na jinsi uvamizi huo ulivyotekelezwa na mwishowe akaitisha kuondolewa kwa wanajeshi wa Marekani nchini humo.

Alishinda tena kwa urahisi uchaguzi wa useneta 2006.

Kuwania urais

Mwaka 2008 aliwania uteuzi wa kuwa mgombea urais wa chama cha Democratic. Hata hivyo, wakosoaji wake - baadhi kutoka hata kwenye chama chake - walimchukulia kama mtu wa kuwagawanya watu na ambaye hawezi kuungwa mkono na Wamarekani wengi.

Mwishowe, Barack Obama alishinda uteuzi na kisha uchaguzi mkuu.

ALimteua waziri wa mambo ya nje katika juhudi za kuziba ufa uliokuwa umejitokeza chama cha Democratic wakati wa kampeni za uchaguzi wa mchujo.

Maelezo ya picha,

Bi Clinton alikubali kumtumikia Barack Obama serikalini

Wakati wa miaka minne aliyohudumu, Bi Clinton alizuru nchi 112, safari nyingi kushinda waziri yeyote wa mambo ya nje aliyemtangulia.

Bi Clinton alitumia nafasi yake kutetea haki za wanawake na haki za kibinadamu. Aidha, aliongoza mpango wa Marekani kuchukua hatua kutokana na misukosuko ya kisiasa nchi za Kiarabu na pia kuingilia kijeshi nchini Libya 2011.

Wizara ya mambo ya nje ilikosolwa vikali baada ya kushambuliwa kwa afisi za kibalozi za Marekani Benghazi mwezi Septemba 2012,. Balozi wa Marekani ni miongoni mwa waliouawa.

Kwenye kikao cha kamati ya bunge, moja ya shughuli zake rasmi alizofanya hadharani kama waziri wa mambo ya nje, Bi Clinton alikubali lawama kutokana na upungufu wa kiusalama katika afisi hizo za ubalozi. Hata hivyo, alisema hakupokea ombi la kuimarisha usalama katika ubalozi huo mapema.

Alirejea kwenye bunge la Congress kuhojiwa kuhusu shambulio hilo Oktoba 2015. Licha ya kuhojiwa kwa zaidi ya saa 11 na kamati maalum, hakuna maelezo mapya yaliyopatikana.

Baada ya kuacha uwaziri, Bi Clinton aliendelea kujitokeza hadharani na kutoa hotuba ingawa si mara nyingi.

Kabla ya kutangaza kwamba angewania urais kulitokea tuhuma kwamba alivunja sheria alipokuwa waziri wa mambo ya nje kwa kutumia barua pepe ya kibinafsi kutuma na kupokea barua pepe rasmi za kikadhi, baadhi zikiwa na habari za umuhimu mkubwa kiusalama.

Maelezo ya picha,

Hillary Clinton akishiriki mdahalo na mpigani wake mchujo wa Democratic Seneta Bernie Sanders

FBI walitangaza kwamba hawangemfungulia mashtaka Bi Clinton, lakini wakasema Bi Clinton na wafanyakazi wake walikosa kumakinika walipokuwa wanashughulikia habari na maelezo muhimu ya taifa yanayofaa kuwa siri kuu.

Utata wa kisheria kuhusu kashfa hiyo ya barua pepe uliathiri kampeni za Bi Clinton mapema wakati wa mchujo na hata alipoidhinishwa, huku kura za maoni zikidokeza kwamba bado kuna wapiga kura wanaotilia shaka kuaminika kwake.

Seneta wa Vermont Bernie Sanders alikabiliana naye vikali kwenye mchujo, kuliko ilivyotarajiwa lakini mwishowe alishinda.

Alipanda kwenye kura za maoni baada ya kuidhinishwa kuwania urais, na kuwa mwanamke wa kwanza kuteuliwa na chama kikubwa Marekani kuwa mgombea.

Lakini ameendelea kukabiliwa na mpinzani wake wa Republican Donald Trump na alishuka zaidi Septemba alipowakosoa wafuasi wa Bw Trump na kusema ni "kapu la watu wa kusikitisha" na wasioweza kuokolewa.

Siku mja baadaye, aliugua wakati wa sherehe ya kuwakumbuka waathiriwa wa shambulio la 9/11 na baadaye maafisa wake wakasema aliugua nimonia au kichomi. Hata hivyo, alirejea mwenye nguvu na amekuwa akiongoza pakubwa kwenye kura za maoni dhidi ya Bw Trump tangu wakati huo.