Uchunguzi Peru baada ya vyura 10,000 kufa

Vyura wa Titicaca wanakabiliwa na hatari ya kuangamia

Chanzo cha picha, Nature Picture Library/Alamy

Maelezo ya picha,

Vyura wa Titicaca wanakabiliwa na hatari ya kuangamia

Mamlaka ya mazingira nchini Peru inachunguza chanzo cha vifo vya vyura 10,000 ambao mizoga yao imepatikana katika mto unaomwaga maji katika ziwa Titicaca.

Kundi moja la kutetea uhifadhi wa mazingira kwa jina Committee Against the Pollution linasema uchafuzi katika mto Coata ndio uliosababisha vifo hivyo.

Linasema serikali imepuuzilia mbali malalamiko kuhusu ujenzi wa bwawa la kusafisha maji taka eneo hilo.

Vyura wa Titicaca, ambao huishi katika maji yasiyo na chumvi, wamo hatarini ya kuangamia.

Vyura hao, ambao kitaalamu hujulikana kama Telmatobius culeus, hupatikana katika ziwa hilo ambalo hupatikana mpakani wa nchi za Peru na Bolivia pamoja na mito inayomwaga maji katika ziwa hilo.

Vyura hao huliwa na binadamu.

Wanaharakati wa Committee Against the Pollution majuzi walibeba mizoga ya vyura 100 na kuiweka uwanja mkubwa katika mji mkuu wa eneo hilo, Puno kuishinikiza serikali kuchukua hatua.