Sudan Kusini yamuonya Riek Machar kutorudi hadi 2018

Riek Machar
Image caption Riek Machar

Msemaji wa rais nchini Sudan Kusini ametoa wito kwa aliyekuwa makamu wa rais wa taifa hilo Riek Machar ambaye yuko mafichoni huko Afrika Kusini baada kutoroka Juba mnamo mwezi Julai kutorudi nchini humo hadi 2018.

Ateny Wek Ateny aliambia BBC kwamba anamuonea huruma Bwana Machar ambaye ameambia BBC kwamba nusu ya taifa hilo lipo chini ya mikono ya vikosi vya waasi wa SPLM-IO.

''Serikali inadhibiti asilimia 95 ama 99.9 ya taifa.Anajaribu kuwadanganya wale ambao hawajui ramani ya Sudan Kusini.

Nilimuonea huruma,kwa sababu iwapo wanajeshi wake wanadhibiti nusu ya taifa ..asingetoroka Juba''.

Alipoulizwa iwapo bw Machar bado angeweza kushauriana kuhusu makubaliano ya amani na rais Salva Kiir,msemaji huyo alisema kwamba awamu hiyo imepitwa na wakati na serikali haimtambui kuwa kiongozi wa SPLM-IO.

Kuhusu kuapa kwa Machar kwamba atarudi Sudan Kusini,bw Ateny alikuwa na haya ya kusema:Iwapo anataka kurudi nchini Sudan Kusini,basi anaweza kurudi baada ya 2018 ,wakati serikali ya mpito itakuwa imekamilikana na uchaguzi umeitishwa.