Wana anga wawili wa China wafika anga za juu

Jin Haipeng na Chen Dong wakiwa Tiangong 2 19 Oktoba 2016 Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Runinga ya taifa iliwaonyesha moja kwa moja Jing Haipeng (kushoto) na Chen Dong wakipunga mikono walipokuwa wakiingia katika Tiangong

Wana anga wawili kutoka China wamefika katika kituo cha anga za juu cha taifa hilo cha Tiangong 2, ambapo watakaa kwa siku 30 wakifanya utafiti.

Walikuwa wameabiri chombo cha anga za juu kwa jina Shenzhou-11 ambacho kilirushwa kwa roketi kutoka kaskazini mwa China siku ya Jumatatu.

Walifika katika Tiangong 2 saa tisa na dakika 24 usiku wa manane saa za Beijing Jumatano.

Jing Haipeng na Chen Dong watakaa siku 30 wakifanya utafiti na majaribio mbalimbali.

Kitakuwa kipindi kirefu zaidi kwa wataalamu kutoka China kukaa nga za juu.

Chombo chao kiliungana na mitambo ya Tiangong 2 wakiwa umbali wa kilomita 393 juu ya dunia. Shughuli hiyo ambayo ilisimamiwa kwa mitambo kutoka ardhini ilichukua mwendo wa saa mbili hizi hadi vyombo hivyo vikaunganishwa salama, vyombo vya habari Uchina vimesema.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Walifika usiku wa manane saa za Beijing

Wakiwa huko anga za juu, wataalamu hao wawili watafanya utafiti na majaribio kuhusu mambo mbalimbali yakiweko ukuzaji wa mimea kama vile mpunga. Aidha, watachunguza mabadiliko kwenye miili yao.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Chombo cha Shenzhou-11 kilipaa kutoka kaskazini mwa China Jumatatu

China ndiyo nchi ya tatu, baada ya Urusi na Marekani, kutuma binadamu anga za juu kwa kutumia watu kwa kutumia roketi zake binafsi.

China ilizuiwa kutumia Kituo cha Kimataifa cha Anga za Juu (ISS) kutokana na dhana kwamba mpango wake wa anga za juu pia unakusudia kujiimarisha kijeshi.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii