Mfalme wa Morocco akutana na Kagame

Mfalme Mohamed VI Haki miliki ya picha Ikulu, Rwanda
Image caption Mfalme Mohamed VI anatarajiwa pia kuzuru Tanzania na Ethiopia

Mfalme wa Mohamed VI wa Morocco ameanza ziara ya siku tatu nchini Rwanda, ambapo baadaye anatarajiwa pia kuzuru Tanzania na Ethiopia.

Akiwa nchini Rwanda Mfalme wa Morocco atafanya mazungumzo na mwenyeji wake rais Paul Kagame ambayo yanajikita katika maswala la kisiasa, na kuimarisha uhusiano wa nchi mbili hususan kibiashara.

Rwanda imetajwa kuwa na nafasi kubwa katika kushawishi mataifa ya Afrika kuikubalia Morocco kurejea katika umoja wa Afrika.

Morocco ilibainisha rasmi kutaka kurejea katika umoja wa afrika kwenye kikao cha umoja huo kilichofanyika nchini Rwanda mapema mwezi wa saba mwaka huu.

Viongozi wote wawili, Kagame na Mohamed VI, walikuwa wamelizungumzia suala hilo walipokutana nchini Morocco kabla ya kikao hicho cha AU mjini Kigali.

Haki miliki ya picha Ikulu, Rwanda
Image caption Morocco inataka kuruhusiwa kurejea AU

Morocco ilijitoa katika jumuiya ya Afrika mwaka 1984 baada ya jumuiya hiyo kutangaza kuitambua Jamuhuri ya watu wa Sahara inayopigania kujitenga na utawala wa Morocco.

Mbali na swala hilo, Rwanda na Morocco wanataraji kutia saini mapatano ya ushirikiano kibiashara.

Makampuni kadhaa ya Morocco yameomba kuwekeza biashara zao nchini Rwanda ambapo tayari baadhi ya benki zimeanza kufanya kazi.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii