Rwanda yatia saini makubaliano na Morocco

Rais Kagame wa Rwanda
Image caption Rais Kagame wa Rwanda

Rwanda na Morocco wametia saini mapatano kadhaa ya ushirikiano kisiasa,kiuchumi na kijamii.Mapatano hayo yamesainiwa wakati wa ziara ya mfalme wa Morocco Mohamed wa sita nchini Rwanda.

Ni mapatano 16 ya ushirikiano baina ya Rwanda na Morocco ndiyo yaliyosainiwa.Mapatano hayo yamesainiwa wakati wa ziara ya mfalme wa Morocco Mohamed wa sita nchini Rwanda.

Mapatano hayo ni katika nyanja tofauti zikiwemo kisiasa na diplomasia ambapo nchi mbili zimekubaliana kuondoa visa kwa viongozi wa nchi zote mbili;hii ikiwa ni njia ya kuimarisha wazo la umoja wa afrika la nchi zote za bara kutumia paspoti moja.

Sehemu kubwa ya mapatano hayo inahusu ushirikiano katika sekta ya uwekezaji ,utalii na kutoa nafasi kwa mashirika ya ndege kutoka pande mbili kuanzisha misafara yake katika kila nchi.

Makampuni kadhaa ya Morocco yameomba kuwekeza biashara zao nchini Rwanda ambapo tayari baadhi ya benki zimeanza kufanya kazi.

Kisiasa,Rwanda imetajwa kuwa na nafasi kubwa katika kushawishi mataifa ya Afrika kuikubalia Morocco kurejea katika Umoja wa Afrika.

Morocco ilibainisha rasmi kutaka kurejea katika Umoja wa Afrika kwenye kikao cha Umoja huo kilichofanyika nchini Rwanda mapema mwezi wa saba mwaka huu.

Viongozi wote wawili,Kagame na Mohamed VI walikuwa wamelizungumzia swala hilo walipokutana nchini Morocco kabla ya kikao hicho cha AU mjini Kigali.

Morocco ilijitoa katika jumuiya ya Afrika mwaka 1984 baada ya jumuiya hiyo kutangaza kuitambua Jamuhuri ya watu wa Sahara inayopigania kujitenga na utawala wa Morocco.

Mfalme wa sita wa Morocco anatarajiwa pia kuzitembelea Tanzania na Ethiopia.