Gaddafi: Kumuomboleza 'masihi wa Afrika'

Muammar Gaddafi Haki miliki ya picha Getty Images

Leo ni miaka mitano tangu kuuawa kwa kiongozi wa muda mrefu wa Libya, Muammar Gaddafi ambaye alituhumiwa na nchi za Magharibi na mashirika ya kutetea haki za kibinadamu kwa ukatili na kukandamiza wapinzani.

Utawala wake uliangushwa kufuatia mashambulio ya ndege za kivita za nchi za Magharibi chini ya mwavuli wa shirika la kujihami la Nato.

Baada ya kuuawa kwake, maelfu ya watu walishangilia kote nchini Libya.

Lakini kadiri miaka ilivyosonga, watu wameanza kumkumbuka na kumuenzi hasa baada ya taifa la Libya kutumbukia katika misukosuko ya kisiasa na vita.

Maelfu ya watu wamekuwa wakitumia taifa hilo kujaribu kufika Ulaya, baadhi wakifariki katika bahari ya Mediterranean. Mataifa ya Ulaya pia yanalalamikia ongezeko la wahamiaji.

Katika nchi za Afrika, wakazi wa nchi ambazo Kanali Gaddafi kwa njia moja au nyingine alichangia kisiasa au kwa miradi ya ujenzi, anakumbukwa.

Mfano nchini Ghana, mwandishi wa BBC Jake Wallis Simons anasema hakuenda mbali sana kabla ya kukutana na watu ambao bado wanaomboleza kifo cha Gaddafi.

Karim Mohamed, 46, ambaye ni fundi wa nguo alisema Gaddafi alikuwa kama "masihi wa Afrika".

Alikuwa ameishi Libya wakati wa utawala wa Gaddafi.

"Nchini Libya, kila mtu alikuwa na furaha," anasema.

"Nchini Marekani, kuna watu wanaolala chini ya madaraja. Lakini Libya hilo halikufanyika. Hakukuwa na ubaguzi, hakukuwa na shida, hakuna lililokosekana. Kazi ilikuwa nzuri na kulikuwa na pesa pia. Maisha yangu yako yalivyo sasa kwa sababu ya Gaddafi. Alikuwa masihi wa Afrika."

Jake Wallis Simon alikutana na wanaume wengine wawili ambao pia waliunga mkono Karim.

Muammar Gaddafi

1942

Azaliwa eneo la Sirte, Libya

  • 27 Umri wake alipoingia madarakani kupitia mapinduzi mwaka 1969.

  • Juni 2011 Mahakama ya ICC yatoa kibali cha kukamatwa kwake

  • 21 Okt 2011 Auawa na waasi akijaribu kutoroka Sirte

"Gaddafi alikuwa mtu mzuri," alisema Mustafa Abdel Momin, 36, mfanyakazi wa mjengo ambaye alifanya kazi nchini Libya kwa miaka saba.

"Hakumtapeli yeyote. Alikuwa mtu mzuri sana, bora zaidi."

"Ilikuwa na maana gani kumuua?" aliongeza Eliyas Yahya, imam wa eneo hilo.

"Mnaua mtu kutatua tatizo na sasa matatizo yamezidi. Mbona kumuua Gaddafi?"


Haki miliki ya picha Thinkstock

Gaddafi alikuwa mtawala wa kiimla lakini utajiri uliotokana na uthabiti wa utawala wake uliwavutia watu wengi kutoka nchi nyingine za Afrika walioenda kutafuta kazi.

Karim, Mustafa na Eliyas ni wachache tu kati ya maelfu ya Waafrika walitumia pesa walizopata wakifanya kazi Libya kujiimarisha kimaisha nyumbani.

Karim alimuonyesha Jake jumba la manispaa ambalo linamilikiwa na Sheikh Swala, aliyeanzisha biashara nyingi akitumia pesa alizopata baada ya kufanya kazi Libya. Jumba hilo na vyumba 30 vya kulala. Na bila Gaddafi, hangeliweza kulijenga.

Katika eneo alilotembezwa, ni nadra siku hizi kupata nyumba mpya zikijengwa. Kuna nyumba ambazo hazikuwa zimekamilishwa kujengwa Gaddafi alipoondolewa madarakani, hazijawahii kuendelezwa tangu wakati huo.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Wahamiaji wengi kutoka nchi za Afrika walilazimika kutoroka Libya mwaka 2011

Amadu, 36, pia alikuwa ameenda Libya mwaka 2010. Kufikia 2011, vita vilipoyozuka, alikuwa ameweka akiba $3,500 (£2,300).

Makabiliano yalipoanza, alikuwa bandarini Tripoli. Alilazimika kukimbilia usalama na alijifungia chumbani siku kadha. Alifanikiwa kurejea Ghana salama lakini hakuweza kubeba pesa alizokuwa ameweka akiba.

Ndoto yake ya maisha bora ilikufa na Gaddafi.

Nchini Ghana, Mustafa anasema hakuna kazi na vijana wengi wanahangaika.

"Baada ya kifo cha Gaddafi, ni shida kila pahali. Ukosefu wa ajira umezidi, hakuna cha kufanya. Tunaishia kujiingiza katika uhalifu kujitafutia pesa, au tunajaribu kwenda Ulaya," anasema Mustafa.

Wenzake walikubaliana naye: "Sasa ni kwenda Ulaya, Ulaya, Ulaya, popote duniani," alisema Eliyas. "Wengine wanaenda Brazil, iwapo wana uwezo wa kifedha. Lakini wengine wote, wanaenda Ulaya."

Kabla ya Gaddafi kuuawa, aliuonya Umoja wa Ulaya kwamba serikali yake ikisambaratika, zaidi ya wahamiaji milioni mbili wangefika katika fuo za Ulaya.

Huenda alikuwa dikteta zaidi ya kuwa mkombozi. Lakini ni kana kwamba alikuwa sahihi kuhusu hilo la wahamiaji.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Muammar Gaddafi akiwa Accra, Ghana mwaka 2007

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii