Afrika Kusini kujiondoa mahakama ya ICC

Omar al Bashir Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Bashir alilakiwa na wafuasi wake uwanja wa ndege Khartoum baada ya kurejea kutoka Afrika Kusini

Afrika Kusini imeanzisha mchakato wa kujiondoa kutoka uanachama wa mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita.

Wanadiplomasia wa Afrika kusini wamearifu Umoja wa Mataifa juu ya uamuzi huo na kuilaumu ICC kwa kuzilenga zaidi nchi za Afrika.

Jaji wa zamani wa Afrika Kusini Richard Goldstone, ambaye amehusika katika mifumo ya haki ya kimataifa, ameambia BBC kwamba amesikitishwa sana na uamuzi huo.

"Ni siku ya huzuni sana kwangu," amesema.

Ameeleza kuwa Afrika Kusini ilitekeleza mchango muhimu katika kuundwa kwa mahakama hiyo.

Aidha, amepuuzilia mbali tuhuma kwamba ICC inaonea mataifa ya bara la Afrika.

Uamuzi wa Afrika kusini kujiondoa ulitokana na shinikizo ilikumbana nazo mwaka uliopita za kuitaka imkamate rais wa Sudan Omar al Bashir wakati wa mkutano wa muungano wa nchi za Afrika mjini Johannesburg.

Waziri wa haki Michael Masutha amesema mzozo huo kuhusu Bw Bashir uliifanya nchi hiyo kutafakari upya manufaa na madhara ya kusalia kwenye mahakama hiyo.

Bw Masutha amesema Afrika Kusini imeombwa mara kadha kupatanisha katika mazungumzo ya kutafuta amani na hilo huhitaji kukutana na pande zinazozozana.

Amesema kuwajibishwa na ICC kunaweza kukaathiri uwezo wa Afrika Kusini kupatanisha katika mizozo inayoyakumba mataifa barani Afrika.

Septemba mwaka jana, mahakama nchini nchini Afrika Kusini iliinyima serikali ya nchi hiyo ruhusa ya kukata rufaa uamuzi ulioishutumu kwa kukosa kumkamata Bw Bashir alipohudhuria kongamano hilo mwezi Juni mwaka 2015.

Serikali ilitaka kukata rufaa uamuzi wa Mahakama Kuu ikisema Bashir alikuwa na kinga ya urais kwa sababu yeye ni kiongozi wa taifa.

Lakini Jaji Hans Fabricius alisema rufaa hiyo haiwezi kufanikisha chochote.

Aliongeza kuwa Afrika Kusini ni mwanachama wa Mkataba wa Roma uliounda mahakama hiyo, na kwamba mkataba huo unabatilisha sheria zozote ambazo huenda zingempa kinga Bashir asikamatwe na kushtakiwa.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Wafuasi wa Bashir wakibeba mfano wa jeneza la ICC kuikejeli mahakama hiyo baada ya Bw Bashir kurejea Khartoum

Kiongozi huyo wa Sudan amekuwa akisakwa na Mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ICC kwa tuhuma za kutekeleza mauaji ya halaiki na makosa ya uhalifu wa kivita Darfur.

Kiongozi huyo aliyechukua mamlaka kupitia mapinduzi ya kijeshi mwaka 1989 amekanusha madai hayo.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii