Jaji Mexico akataa rufaa ya El Chapo

Joaquin "El Chapo" Guzman Haki miliki ya picha AFP
Image caption Guzman alikamatwa tena Januari baada ya kuwa mtoro kwa miezi sita

Jaji nchini Mexico ametupilia mbali rufaa iliyokuwa imewasilishwa na mlanguzi wa dawa za kulevya Joaquin "El Chapo" Guzman kupinga kupelekwa Marekania akajibu mashtaka.

Wizara ya mambo ya nje ya Mexico iliidhinisha El Chapo akabidhiwe kwa maafisa wa Marekani lakini mawakili wa mlanguzi huo wamekuwa wakipinga uamuzi huo mahakamani.

Sasa, wamesema watakata rufaa katika mahakama ya juu.

Mkuu huyo wa genge la walanguzi wa mihadarati la Sinaloa alikamatwa mwezi Januari miezi sita baada yake kutoroka gerezani kwa kupitia njia ya chini ya ardhi iliyochimbwa hadi kwenye seli yake gerezani.

Alikuwa tayari ametoroka kutoka gereza la ulinzi mkali mara moja awali, na akakaa miaka 13 akitafutwa sana na maafisa wa usalama.

Kamishna mkuu wa usalama wa Mexico Renato Sales Heredia amesema kwenye mahojiano na kituo kimoja cha runinga kwamba Mexico inatarajia kumhamishia Marekani mshukiwa huyo "Januari au Februari".

Kupitia taarifa, afisi ya mwanasheria mkuu imesema jaji huyo "ameamua kukataa kinga" iliyokuwa imeombwa na Guzman.

Andres Granados, mmoja wa mawakili wa Guzman, amesema sasa watakata rufaa Mahakama ya Juu zaidi na ikibidi watawasilisha kesi hizo kwa Tume ya Haki za Kibinadamu ya Nchi za Amerika.

"Hatujashindwa," ameambia shirika la habari la AFP.

Mexico ilikubali kumkabidhi Guzman kwa Marekani mwezi Mei baada ya kupata hakikisho kwamba hatakabiliwa na hukumu ya kifo.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii