UN: Vikosi vya usalama DRC vimehusika na mauaji wakati wa maandamano

Maandamano ya kuipinga serikali mwezi uliopita Kinshasa Haki miliki ya picha Reuters

Uchunguzi wa kina wa taasisi ya Umoja wa mataifa ya haki za binaadamu (UNJHRO) imewashutumu wanajeshi, polisi na walinzi wa rais katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kwa visa vingi vilivyoripotiwa vya ukiukaji wa haki za binaadamu wakati wa ghasia zilizotokea katika maandamano ya siku mbili katika mji mkuu Kinshasa, mwezi uliopita

Serikali imesema watu 32 wamefariki, lakini ripoti ya Umoja wa mataifa inasema idadi ya waliokufa ni kubwa zaidi.

'Takriban watu 53, wakiwemo wanawake 7 na watoto wawili waliuawa'.

'Huenda idadi ikawa kubwa zaidi, kwasababu shirika hilo la Umoja wa mataifa UNJHRO lilikatazwa mara kadhaa kuingia katika baadhi ya maeneo wakati wa uchunguzi wake , yakiwemo maeneo ya vizuizi na maenoe ambapo wangepata taarifa zaidi'.

Maafisa walitekeleza 'mauaji ya watu takriban 18 kiholela wakiwemo 16 waliopigwa risasi na kuuawa miongoni mwa idadi jumla ya waliouawa', ripoti hiyo inaongeza.

Ukigusia siku ya kwanza ya maandamano hayo ya kupinga serikali Septemba 19, Uchunguzi umeleeza kuhusu ripoti zinazolingana za 'kusambazwa kwa mapanga na pesa na maafisa wa serikali kwa vijana 100 kwa lengo la kuchafua maandamano hayo'.

Haki miliki ya picha Getty Images

Ripoti hiyo pia imetaja ghasia na uporaji uliotekelezwana waandamanji. Na kuwa katika siku io hiyo ya kwanza ya maandamano, waandamanaji waliwapiga maafisa wanne wa polisi hadi kuwaua, Huku mwili mmoja ukiteketezwa moto.

Uchaguzi uliotarajiwa mwezi ujao umeahirishwa hadi 2018, huku wakosoaji wakimshutumu rais Joseph Kabila kwa kujaribu kusalia madarakani kupita muhula wake wa mwisho.